
“Msimu huu nataka kufunga mabao 15, na sasa nimeshatia kambani mawili kwa hiyo mzigo unazidi kupungua taratibu, kama mambo yakienda vyema basi yanaweza kuzidi. Kwa sasa napambania kufika hapo.
“Nafasi yangu uwanjani kwa sasa nacheza namba 10 na hata kocha anavyonitumia ni tofauti na msimu uliomalizika, kuna majukumu yamepungua,” amesema Fei Toto.
Kiungo mahiri wa Azam FC, Feisal Salum ‘Fei Toto’, ameweka wazi malengo yake ya msimu huu, akisema anataka kufunga mabao 15 tu, huku akimpa maua kocha Florente Ibenge.
Fei Toto ambaye amewahi kuichezea Yanga, huu ni msimu wake wa tatu ndani ya Azam FC akifunga mabao mawili kwenye ligi, huku msimu uliopita akiibuka kinara wa pasi za mwisho kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa nazo 13 pamoja na kufunga mabao manne.
Kabla ya hapo, msimu wa kwanza ndani ya Azam 2023-2024, alifunga mabao 19 na pasi za mwisho saba.
Akizungumza na Mwananchi, Fei Toto amesema, msimu huu hana mpango kabisa na rekodi za pasi za mwisho huku akitaka kufunga mabao zaidi.
Alisema mabao 15 kwake siyo machache ingawa ameshawahi kufunga zaidi ya hayo, hivyo kila msimu huwa unakuja na mipango yake na huo ndio alionao kwa sasa.
Ibenge hatari
Fei Toto amesema, uwepo wa kocha mkubwa kama Ibenge ndani ya Azam unaongeza kitu kikubwa kwa timu, lakini hata kwake anaamini sana kwamba kuna vitu vitaongezeka.
“Makocha wote ni wazuri, ila wanatofautiana na sasa tuna Ibenge, kiukweli ni kocha mwenye mbinu nzuri anayeamini katika juhudi za mchezaji kuanzia mazoezini.
“Naiona Azam ya tofauti msimu huu kama kwa pamoja tutaungana kuhakikisha tunaipeleka timu mbali hasa katika michuano ya kimataifa na ya ndani na huo uwezo tunao,” amesema.
Huu ukiwa ni msimu wa tatu Fei Toto ndani ya Azam, amefunga jumla ya mabao 25 kwenye Ligi Kuu Bara na pasi za mwisho 20, huku ikielezwa katika mkataba wake mpya aliosaini hadi 2027, kuna kipengele cha bonasi endapo akifunga mabao mengi zaidi.
Takwimu Fei Toto
Msimu Mabao pasi za mwisho
2023-2024 19 07
2024-2025 4 13
2025-2026 2 00