Dar es Salaam. Kwa miaka zaidi ya 15, Salama Jabir a.k.a Ece Jay amekuwa akitangaza katika televisheni na ni miongoni mwa watangazaji waliotokea kupendwa zaidi na vijana kwa namna anavyojipambanua katika mambo yake.

Baadhi ya watu wamekuwa wakimwogopa kwa namna anavyouliza maswali na kukosoa lakini cha kushangaza, anaeleza kuwa yeye ni mtu mwenye aibu sana ila inapofika muda wa kazi anaiweka pembeni.

Kazi yake tangu mwanzo imekuwa na mchango mkubwa katika ukuaji wa tasnia ya burudani nchini hasa upande wa Bongofleva, muziki unaopendwa na vijana wengi. Je, Salama Jabir ni nani?, na mchango wake katika tasnia ni upi?

Salama ni mtoto wa mwisho kwenye famili yao akiwa amezaliwa Zanzibar. Katika kuhakikisha anasoma aliweza kuishi kwenye mikoa ya Tanga na Dar es Salaam hadi pale alipofanikiwa kumaliza elimu ya sekondari.

“Mimi nilitoka Zanzibar kwa mara ya kwanza kuja Bara kwa sababu walipenda uchezaji wangu, waliponiona kwenye UMISETA. Pia nilikuwa nacheza table tennis na huko ndipo nilikutana na AY kwenye mashindano Arusha,” anaeleza Salama.

Akiwa na umri wa miaka 17/18 wakati huo anaishi na dada yake alisikia Times FM wanasaka watangazaji ndipo akaanza mchakato wa kuhakikisha anafanikiwa kufanya kazi kwenye redio hiyo kwa sababu alikuwa na ndoto hiyo.

Kwa bahati nzuri alikuwa anajuana na msanii Soggy Doggy ambaye alikuwa anafanya kazi Times FM kwa wakati huo, ndipo alipomtafuta na kumueleza dhamira yake.

Haikuchukua muda, Salama akaanza kazi ya redioni na alikuwa akitangaza kipindi cha jioni. Hata hivyo, alifanya kazi hapo kwa kipindi cha takribani miezi mitatu, kisha akatimkia East Africa Radio.

Hii ni baada ya Ray C kuacha kazi kwenye redio hiyo ili kufanya muziki ndipo Salama akachukua nafasi hiyo. Ray C naye alianzia kwenye utangazaji kama ilivyokuwa kwa Lady Jaydee.

Ndani ya East Africa Radio alikuwa akitangaza kipindi cha usiku. Baadaye kikaanzishwa kipindi cha Planet Bongo kwa upande wa redio na TV. Kuanzishwa kwa kipindi hicho ndio ukawa mwanzo wa Salama kufanya vizuri katika TV.

Kupitia Platnet Bongo alicheza video za wasanii wa Bongofleva na kuzikosoa vilivyo pale alipoona kuna kasoro kitu kilichompatia umaarufu mkubwa na hata nafasi ya kuwa miongoni mwa majaji wa shindano la kusaka vipaji vya uimbaji, Bongo Star Search (BSS).

Akizungumza na gazeti hili, mkongwe wa Bongofleva, Bwana Misosi amesema Salama kupitia Planet Bongo aliwashtua wasanii kujikita katika kuandaa video bora za muziki.

“Amepambana kwa nafasi yake kwa sababu alikuwa anakosoa japo sio kila kitu kilikuwa sawa,” anasema mkali huyo wa kibao, Mabinti wa Kitanga (2003) na kuongeza. “Kwa sisi watu ambao tulikuwa waelewa, hata akikosoa unaona ni mawazo chanya kwa sababu unajua binadamu hapendi kukosolewa lakini ujumla alikuwa yupo sawa.”

“Na amesaidia sana, kwa hiyo watu walikuwa makini wakijua nikipeleka pale video yangu ina kosa hili na hili, basi itaanza kuongelewa hivi na hivi. Kwa hiyo watu walikuwa wanapambana kufanya vitu  vizuri kwa kipindi hicho ingawa teknolojia bado haikuwa kubwa sana.” anasema Bwana Misosi.

Miaka kadhaa ndani ya Planet Bongo na mafanikio makubwa aliamua kwenda kujiendeleza kimasomo nje ya nchi kwa kipindi cha miaka miwili, hivyo kwa wakati huo yupo masomoni alikuwa haonekani tena kwenye TV.

Baada ya kutoka masomoni, ndipo ubunifu wake ulionekana zaidi upande wa vipindi vya TV, kwa kushirikiana na AY na Josh Murunga wakaanzisha kipindi cha Mkasi ambacho kilikuwa kikiruka EATV pia.

Ni kipindi kilichokuja tofauti kutokana na namna ya uwasilishwaji wake. Kitendo cha mtu maarufu kuhojiwa huku ananyolewa nywele au ndevu, na wengine wakitengenezwa nywele zao na kucha, kilivutia.

Kutokana na kufanya vizuri sana na kupendwa na watu, kipindi cha Mkasi kilishinda tuzo mbili kutoka Tuzo za Watu 2015.

Baada ya Mkasi, Salama alikuja na kipindi kingine, Ngaz kwa Ngaz ambacho kilikuja na mwonekano mwingine kabisa machoni kwa watazamaji. Mwonekano (set) wa kama mabati yaliyochakaa kisha kunakshiwa na vipande vichache vya rangi ilivutia zaidi.

Ingawa kilikuwa ni kipindi cha chati za muziki, kiliweza kuwa na vitu vingi mno ikiwamo mahojiano ya aina yake na wasanii, historia zao na vitu vya kustaajabisha, kufundisha na kufurahisha pia.

Haikuishia hapo, alikuja na vipindi vingine viwili, Salama Na Shabiki On Saturday ambacho kinachambua soka, na kutoa nafasi kwa mashabiki kueleza mitazamo yao.

Kwa ujumla katika vipindi vyake vyote amefanya mahojiano na mastaa wa muziki kama AY, Mwana FA, Sugu, Professor Jay, P-Funk Majani, Master J, Juma Nature, Lady Jaydee, Ray C, Fid Q, Dully Sykes, TID n.k.

Wengine ni Alikiba, Diamond Platnumz, Vanessa Mdee, Nahreel, Nandy, Rayvanny, Shilole, Quick Rocka, Lulu Diva, Billnass, Rosa Ree, Jux, Shetta, Ruby, Kusah, Ditto, Dayna Nyange, Madee, Damian Sol, Ommy Dimpoz, Zuchu n.k.

Rapa kutokea Classic Music Group (CMG), Darassa katika mahojiano ya awali, alieleza kuwa kipindi anatafuta kutoka kimuziki, Salama ni kati ya watu wa mwanzo kupokea CD ya kazi yake na kuipa nafasi redioni.

Ikumbukwe, sauti ya wanamke inayosikika mwanzoni mwa wimbo wa Fid Q ‘August 13’ ni ya Salama, na hadi sasa ngoma hiyo iliyotayarishwa Bongo Records na P-Funk Majani, ni miongoni mwa zile zenye intro kali kuwahi kutokea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *