Moshi. Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Moshi (MUWSA) imewataka wakazi wa Manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, ambao wamepitiwa na mtandao wa maji taka, kuwasilisha maombi ya kuunganishwa na mfumo huo ili kuboresha usafi wa mazingira na kulinda afya za wananchi.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999, mtandao wa maji taka wa MUWSA umeongezeka kutoka kilomita 13 hadi kufikia kilomita 102, huku idadi ya wateja ikipanda kutoka 300 hadi zaidi ya 3,700.

Akizungumza jana, Oktoba 10, 2025, Meneja Msimamizi wa Huduma za Majitaka na Usafi wa Mazingira wa MUWSA, Philbert Nyangwe, amesema mamlaka hiyo inaendelea kupanua huduma kwa kujenga miundombinu mipya katika maeneo mbalimbali ya manispaa hiyo.

“Hivi karibuni tumekamilisha mradi wa ujenzi wa mtandao wa maji taka wa kilomita nane kutoka Kiwanda cha Ngozi cha Kilimanjaro hadi mabwawa ya majitaka. Mradi huu umepita katika kata nne muhimu na unatarajiwa kunufaisha watu zaidi ya 6,000 pamoja na kiwanda chenyewe,” amesema Nyangwe.

Amesema katika kata 21 za manispaa hiyo, mtandao wa maji taka tayari umepita katika kata 15, hivyo wananchi wanapaswa kuomba kuunganishwa ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na majitaka yanayozalishwa majumbani.

“Majitaka mengi tunayokusanya ni ya majumbani na baada ya kuyatibu, yanakuwa salama kwa mazingira. Tunawahimiza wananchi kufuata utaratibu sahihi wa matumizi ya mfumo huu na kuepuka kutupa taka ngumu kama mizoga au plastiki zinazoweza kuziba mifumo,” amesema.

Nyangwe ameongeza kuwa kwa kata ambazo bado hazijafikiwa na mtandao wa maji taka, huduma hutolewa kupitia magari maalumu ya kuondoa majitaka, huku mipango ikiendelea ya kujenga vituo vipya katika maeneo ya Himo, Msaranga na Hai.

Aidha, amesema MUWSA inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya mifumo ya majitaka na umuhimu wa kulinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya wote.

Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Huduma kwa Wateja wa MUWSA, Mwanandani Mtonyi, amesema wiki ya huduma kwa wateja imekuwa fursa ya kukaribia wananchi na kuboresha huduma kwao.

“Tumeungana na mamlaka nyingine duniani kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja. Tumerejesha huduma kwa baadhi ya wateja waliokuwa wamesitishiwa bila kuwatoza ada ya kurejesha, endapo watalipa madeni yao yote,” amesema Mtonyi.

Ameeleza kuwa MUWSA imeboresha mawasiliano kupitia Call Center na makundi sogozi, hali ambayo imepunguza gharama na muda wa wateja kufuata huduma ofisini.

“Awali tulikuwa tunapokea watu 300 hadi 350 kwa siku, lakini sasa idadi hiyo imeshuka hadi 80 kutokana na wateja wengi kupata huduma kupitia simu,” amesema.

Naye Meneja wa Uchakataji wa Ankara na Udhibiti wa Madeni, Joseph Melkiori, amesema MUWSA inaendelea kuboresha mfumo wa usomaji wa mita kwa kutumia simu za mkononi, hatua inayomwezesha mteja kupata taarifa za matumizi yake papo kwa papo.

“Tunasistiza wateja kulipa ankara zao kwa wakati kwani maji ni uhai. Dhamira yetu ni kuwahudumia kwa ufanisi, uwazi na ubunifu,” amesema Melkiori.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *