Madrid, Hispania. Mambo yanazidi kwenda mrama kwa kiungo wa Real Madrid, Jude Bellingham, baada ya jina lake kuachwa kabisa kwenye kalenda rasmi ya klabu hiyo kwa mwaka 2026 jambo lililowashangaza mashabiki wengi wa Los Blancos.

Bellingham (22), ambaye mwaka jana picha yake ilitumiwa kwenye kampeni za masoko za Real Madrid kama mchezaji tegemeo, safari hii hajatajwa kabisa katika kalenda hiyo inayouzwa kwa Paundi 10.99. Badala yake, picha zinazotumika ni za wachezaji kama Arda Güler, Dean Huijsen na Kylian Mbappé pamoja na wakongwe Dani Carvajal na Éder Militão.

Kukosekana kwake kunakuja kipindi ambacho nafasi yake ya kwanza kikosini imeanza kuyumba chini ya kocha Xabi Alonso, kufuatia kurejea kwake kwa taratibu baada ya upasuaji wa bega.

Tangu arudi uwanjani mwezi Septemba, ameanza kwenye mechi moja pekee ile ya kufungwa mabao 5-2 na Atletico Madrid, kabla ya kuanza kutumika kama mchezaji wa akiba kwenye michezo iliyofuata.

Ingawa Alonso amesisitiza kuwa anathamini ubunifu wa Bellingham, inaonekana hataki kuivunja safu ya kiungo ambayo kwa sasa ipo kwenye kiwango bora.

Kukosa nafasi Madrid na England

Mbali na changamoto za klabuni, Bellingham pia ameachwa nje ya kikosi cha England kilichoitwa na kocha Thomas Tuchel kwa michezo ya kimataifa ya mwezi Oktoba.

Tuchel alisema nyota huyo bado hajapata ufiti kamili na anahitaji muda zaidi kurudisha kiwango chake.

Hii imeongeza msongo kwa Bellingham ambaye miezi michache tu iliyopita alikuwa mchezaji asiyeweza kuguswa, akiwa kipenzi cha mashabiki wa Madrid na England.

Kuachwa kwake kwenye kalenda ingawa ni jambo la kibiashara limechukuliwa kama ishara ya kushuka kwa hadhi yake ndani ya klabu. Tangu ujio wa Alonso, nafasi yake katika kiungo imekuwa ngumu zaidi kutokana na kuibuka kwa vijana kama Franco Mastantuono na Güler.

Alexander-Arnold naye aachwa nje

Siyo Bellingham pekee aliyeachwa kwenye kalenda hiyo. Trent Alexander-Arnold, beki mpya wa kulia aliyesajiliwa kutoka Liverpool majira ya kiangazi, pia picha yake haipo.

Arnold (26) alihamia Madrid kwa ada ya Pauni milioni 8.4 lakini amekuwa akikabiliwa na majeraha tangu aanze maisha yake Bernabéu. Alipata jeraha la msuli wa paja kwenye mchezo wake wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Marseille, jambo lililomweka nje kwa wiki sita hadi nane.

Kutokana na majeraha yake, Alonso amekuwa akilazimika kumtumia mkongwe Carvajal kucheza nafasi hiyo ya beki wa kulia.

Kwa sasa, mashabiki wa Madrid wanasubiri kuona kama Bellingham ataweza kurejea kwenye kiwango chake cha juu, au kama kuachwa kwenye kalenda ni ishara ya mwanzo wa mwisho wa enzi yake Bernabéu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *