Dodoma. Serikali imewataka watafiti wa taasisi za elimu ya juu nchini kutumia fursa ya Tuzo za Umahiri wa Tafiti kuongeza ubora wa tafiti zao na kushindana katika viwango vya kimataifa, huku ikitenga Sh1.5 bilioni kwa ajili ya tuzo hizo katika mwaka wa fedha 2026/27.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, Juni 18, 2026, jijini Dodoma wakati wa kutangaza ufunguzi wa dirisha la nne la maombi ya tuzo hizo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika sekta ya utafiti ili kuhamasisha uzalishaji wa maarifa na ubunifu wenye mchango katika maendeleo ya taifa.

Amesema tuzo hizo zilianzishwa Machi 9, 2023, kwa lengo la kuwatambua na kuwazawadia watafiti ambao matokeo ya tafiti zao yamechapishwa katika majarida ya kitaaluma yenye hadhi ya juu duniani.

“Tuzo hizi ni motisha kwa watafiti wetu kuongeza umahiri na kufanya tafiti zinazokubalika katika viwango vya juu vya kimataifa. Tunataka kuona tafiti za Watanzania zikitambulika zaidi duniani,” amesema Profesa Mkenda.

Amesema ushindani huo unahusisha nyanja nne, ambazo ni sayansi asilia na hisabati, afya na sayansi shirikishi, sayansi za wanyama na kilimo, pamoja na uhandisi na teknolojia ya habari na mawasiliano.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, mshindi anaweza kupata hadi Sh50 milioni kwa chapisho moja, huku kiwango hicho kikigawanywa kulingana na mchango wa watafiti walioshiriki katika kazi husika.

Amesema tangu kuanzishwa kwa mpango huo, machapisho 336 yamekidhi vigezo na kushiriki katika ushindani, ambapo machapisho 86 yalifanikiwa kushinda tuzo.

“Jumla ya Watanzania 200 wamenufaika na tuzo hizi tangu kuanzishwa kwake. Watafiti wawili walipata Sh50 milioni kila mmoja baada ya kuandaa na kuchapisha tafiti zao binafsi, huku wengine wakigawana fedha kulingana na ushiriki wao katika machapisho yaliyoshinda,” amesema.

Profesa Mkenda amesema dirisha la kupokea machapisho kwa mwaka huu litakuwa wazi kuanzia Juni 19 hadi Oktoba 31, 2026, na kwamba watafiti wote wenye sifa wanakaribishwa kuwasilisha kazi zao kwa ajili ya ushindani huo.

Amesema maelezo ya kina kuhusu vigezo vya ushiriki, namna ya kuwasilisha maombi na masharti mengine yanapatikana katika tovuti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.

Akieleza sababu za Serikali kuweka mkazo katika machapisho ya majarida ya kimataifa, Profesa Mkenda amesema ubora wa utafiti hupimwa kupitia mchakato wa tathmini ya kitaalamu unaofanywa na wataalamu huru kutoka maeneo mbalimbali duniani kabla ya utafiti kuruhusiwa kuchapishwa.

Amesema majarida makubwa ya kisayansi duniani hupokea maelfu ya machapisho kutoka nchi mbalimbali na kuyafanyia uchambuzi wa kina ili kuhakikisha matokeo ya tafiti hizo yanaaminika na yanaweza kurudiwa na watafiti wengine popote duniani.

“Majarida haya yanafanya tathmini kali sana. Wataalamu kutoka nchi mbalimbali hupewa kazi ya kuchunguza utafiti na kutoa maoni yao kabla ya kuchapishwa. Hivyo, utafiti unapokubaliwa kuchapishwa katika jarida kubwa la kimataifa, unakuwa umepitia mchakato wa uhakiki unaotambulika duniani,” amesema.

Amefafanua kuwa Serikali inalenga kuona watafiti wa Tanzania wakishindana katika kile alichokiita “ligi ya kimataifa ya sayansi”, badala ya kujitathmini ndani ya nchi pekee.

“Tunataka wanasayansi wetu wafanye tafiti zinazokubalika kimataifa na kufanyiwa tathmini kimataifa. Ili kujenga sayansi na teknolojia ya Tanzania, lazima tuingie kwenye ligi ya kimataifa,” amesema.

Amesema ushindani wa kimataifa unasaidia kuongeza hadhi ya watafiti wa Tanzania, kuvutia ushirikiano wa kitaaluma na kuongeza matumizi ya matokeo ya tafiti katika kutatua changamoto za maendeleo.

“Kama watafiti wetu watachapishiana na kujitathmini wenyewe ndani ya nchi pekee, hatutafika mbali. Lazima tushindane na kupimwa kwa viwango vya kimataifa ili kujua ubora wa kazi zetu,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *