Mazishi ya kitaifa ya aliyekuwa kiongozi wa upinzani na waziri mkuu wa zamani nchini Kenya,  Raila Amolo Odinga, yamefanyika  leo katika uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, yakiwaleta pamoja viongozi wa ngazi za juu, wageni wa kimataifa, na maelfu ya wananchi waliofika kumuaga mmoja wa wanasiasa mashuhuri zaidi katika história ya Kenya.

Imechapishwa: Imehaririwa:

Dakika 3 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Jeneza la odinga
Jeneza la odinga REUTERS – Thomas Mukoya

Mazishi hayo yaligubikwa na simanzi na hisia kali, hasa pale wanafamilia waliposimama kutoa hotuba zao za kumkumbuka marehemu.

Mtoto wa kiume wa Raila,  Raila Junior Odinga, alimwelezea babake kuwa nguzo ya familia, rafiki na mlezi wa thamani. Amesema baba yao alikuwa mtu wa imani na ujasiri, ambaye hakusita katika kutetea haki, hata pale alipopoteza uhuru wake binafsi

Raila Junior akinongezena na Oburu Odinga
Raila Junior akinongezena na Oburu Odinga REUTERS – Thomas Mukoya

Aliongeza kuwa urithi wa baba yao utaendelea kupitia vizazi vijavyo, akiahidi kudumisha misingi ya haki, usawa na huduma kwa watu, aliyowaachia.

“Baba alikuwa shujaa, mshauri na rafiki. Nitadumisha yale aliyoyaamini — haki, usawa na huduma kwa wengine,” alisema kwa sauti ya huzuni.

Winnie Odinga – Raila alikuwa rafiki yangu

Winnie Odinga, binti mdogo wa marehemu, alitoa hotuba ya kugusa moyo iliyowaliza wengi. Alisema baba yao alikuwa mtu wa nidhamu, upendo na ucheshi, ambaye aliwafundisha watoto wake kupenda nchi yao na kusimama kwa kile kilicho sahihi.

“Baba alinionyesha kwamba mapenzi kwa nchi si maneno tu, bali ni kujitolea na kufanya kazi kwa ajili ya haki. Uongozi wa kweli ni huduma, si mamlaka,” alisema Winnie.

Alikumbuka pia upendo wa baba yake kwa muziki, familia na timu yake ya Arsenal, akihitimisha kwa maneno mazito:

“Mfalme amefariki, lakini taji linaendelea kuishi.”

Oburu Oginga Odinga – ndugu yalikuwa na msimamo mkali

Kaka mkubwa wa marehemu, Dkt. Oburu Oginga Odinga, alisimulia maisha yao ya utotoni kwa ucheshi, akieleza jinsi Raila alivyokuwa na bidii shuleni na kupenda haki tangu akiwa mdogo.

Alisema Raila alikuwa mtu wa kusimamia ukweli, aliyepinga udanganyifu na uvivu. Kwa uchungu na fahari, aliahidi kuendeleza urithi wa nduguye kisiasa na ndani ya chama cha ODM.

“Ingawa viatu vya Raila ni vikubwa mno, nitaweka juhudi zangu kuendelea na kazi aliyoiamini,” alisema Dkt. Oburu.

Mama Ida Odinga – Raila alikuwa Mpenzi wangu

Mke wa marehemu, Mama Ida Odinga, alisimama kwa huzuni na ujasiri, akiwashukuru Wakenya kwa upendo na maombi yao. Alisema siku hiyo ilikuwa ngumu zaidi maishani mwake, lakini pia ni siku ya shukrani kwa Mungu kwa kumpa  mpenzi wa kipekee.

“Sio kila siku mwanamke husimama mbele ya taifa kumzungumzia mume wake mpendwa. Leo ni siku ya kipekee ya kuaga rafiki na mwenzangu wa maisha,” alisema kwa sauti ya huzuni.

Familia ya Odinga iliwashukuru wananchi kutoka pembe zote za nchi kutoka Turkana hadi Lamu, Isiolo hadi Mandera, na hadi mwambao wa Ziwa Victoria — kwa kusimama nao katika kipindi hiki kigumu.

Walisema kuwa ingawa Raila ameondoka kimwili, urithi wake wa mapambano ya haki, demokrasia na utu utaendelea kuishi ndani ya mioyo ya Wakenya.

“Simba amepumzika, lakini nguvu yake itasikika daima,”  hii ni kauli ya Familia ya Odinga.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *