Nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa zisipolipa michango yao kwa kina na kwa ukamilifu, basi Umoja wa Mataifa ulioanzishwa miaka 80 iliyopita unaweza kufilisika, ameonya Katibu Mkuu António Guterres leo ijumaa wakati akiwasilisha bajeti ya kawaida ya chombo hicho ya mwaka 2026 ya dola bilioni 3.238.
Kiwango hicho kilichofanyiwa marekebisho ni pungufu kubwa kutoka dola bilioni 3.715 zilizokuwa zimeombwa awali na ni punfugu kwa asilimia 15.1 ikilinganishwa na bajeti ya mwaka huu wa 2025.
Akizungumza na wajumbe wa Kamati ya Tano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa yenye wajibu wa kushughulikia fedha na masuala ya utawala ya UN, Katibu Mkuu ameelezea taswira tete na kwamba kucheleweshwa kwa michango na kurejeshwa kwa michango, vinatishia kufuta uwezo wa kifedha wa shirika na kukwamisha operesheni muhimu.
Jengo la makao makuu ya Umoja wa Mataifa lenye bendera za Nchi Wanachama mbele, Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York.
Kupunguza wafanyakazi
Bajeti hii iliyofanyiwa marekebisho inapunguza wafanyakazi kutoka idadi pendekezwa ya awali kwa 2026 ya ajira 13,809 (kati ya hizo 10,667 kutoka ajira za kawaida na 3,142 ajira za kwenye Misheni za Kisiasa) hadi ajira 11,594, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.8 ya punguzo la wafanyakazi ikilinganishwa na mwaka 2025.
Punguzo hilo linamulika Idara kubwa na ajira za kiutawala, huku ikilinda miradi ambayo inahudumia moja kwa moja nchi wanachama—hususan nchi zenye maendeleo duni, LDCs, nchi zisizo na bandari (LLDCs) nchi za visiwa vidogo, (SIDS) na uchechemu kwa maendeleo ya Afrika.
Bajeti ya kawaida, hufadhiliwa kupitia michango ya lazima kutoka nchi wanachama, michango ambayo hulingana na tathmini ya uwezo wa kila nchi kulima, na hujikita kwa program za msingi na operesheni za Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa inayoongozwa na Katibu Mkuu.
Halikadhalika, UN ina bajeti mahsusi ya operesheni za ulinzi wa amani ambayo mzunguko wake ni Julai 1 hadi Juni 30 – ilhali bajeti ya kawaida mzunguko wake ni Januari hadi Desemba.
Madhara ya ukata kuendelea hadi 2027
Katibu Mkuu ameonya kwamba hali ya sasa ya ukata itakuwa na madhara makubwa mwakani na hadi 2027. Kiwango kikubwa cha malimbikizo ya michango mwishoni mwa mwaka jana yakiwa ni jumla ya dola milioni 760, yakigubikwa na marejesho ya lazima ya dola milioni 300 kwa nchi wanachama kuanzia mwaka 2026, kinaondoa takribani asilimia 10 ya fedha za bajeti zilizoko sasa.
“Kucheleweshwa kokote kwa makusanyo ya fedha mwanzoni mwa mwaka, hutulazimu kupunguza matumizi yetu zaidi… na kisha tutalazimika kurejesha dola milioni 600 mwaka 2027, au sawa na asilimia 20 ya bajeti,” amesema Guterres.
“Hii ina maana mbio za kuelekea kufilisika,” amesema Katibu Mkuu akisisitiza udharura wa kupunguza malimbikizo na kusitisha utaratibu wa kurejesha kwa nchi wanachama fedha za bajeti ambazo hazijatumika.
Hatua za awali za kupunguza matumizi zilitoa tu nafuu ya muda mfupi.
Mwaka huu wa 2025 UN iliuanza ikiwa na nakisi ya dola milioni 135, na hadi mwishoni mwa mwezi Septemba, ilikuwa imekusanya asilimia 66.2 tu ya makusanyo yanayotakiwa kutoka nchi wanachama, ikiwa ni pungufu kwa asilimia 78.1 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2024.
Hadi leo hii, ni nchi 136 tu kati ya 193 wanachama wa UN ndio wamelipa kikamilifu michango yao. Baadhi ya wachangiaji zikiwemo Marekani, China, Urusi na Mexico bado hazijakamilisha malipo yao.
Jinsi ya kukabiliana na hali halisi ya kifedha
Bajeti ya 2026 iliyofanyiwa marekebisho inaakisi hali halisi ya kifedha na Mpango wa UN80 unaolenga kufanya Sekretarieti kufanya kazi kwa ufanisi zaidi, kuwa na mnepo na kwa gharama nafuu.
Mikakati ya ufanisi ni pamoja na kuunganisha timu kuwa moja ya kimataifa, kuhamishia majukumu kwenye vituo vya kazi vya gharama nafuu, kuunda majukwaa ya kiutawala ya pamoja jijini New York, Marekani na Bangkok, Thailand.
Vipaumbele muhimu vinasalia, licha ya makato ya majukumu na ajira yatakayofanyika. Mathalani Misheni Mahsusi 37 za Kisiasa zitaendelea, Mfumo wa Waratibu Wakazi utapatiwa dola milioni 53 ilhali Mfuko wa Ujenzi wa Amani dola milioni 50.
Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu, (OHCHR) itapanua ofisi zake za kikanda kwenye miji ya Addis Ababa, Bangkok, Beirut, Dakar, Panama City, Pretoria na Vienna.
Nini kitafuata?
Katika wiki zijazo, Kamati ya Tano itajadili mapendekezo pamoja na Wakuu wa Idara za Sekretarieti ya Umoja wa Mataifa, na mameneja waandamizi wa miradi.
Kamati itawasilisha ripoti yake ya mapendekezo kwenye kikao cha Baraza Kuu, na kupitishwa kwa Bajeti ya UN inatarajiwa kuwa mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka huu wa 2025.
Kuhusu kuimarisha hali ya kifedha ya shirika, katika ripoti yake Guterres amependekea mfumo wa kusitisha urejeshaji wa fedha kwa nchi wanachama wakati wowote ambapo ukata unatishia utekelezaji kikamilifu wa bajeti ya shirika mwaka unaofuatia.
“Wanachama hawakufikia uamuzi, na ripoti ilielekezwa mkutano wa sasa. Kushindwa kufikia makubaliano katika kutatua hali ya kifedha ya shirika kunaweza kuharibu mambo muhimu ya mpango wetu wa kazi,” amesema Katibu Mkuu.