Shinyanga. Uwanja wa Ndege wa Shinyanga kinatarajiwa kupanda hadhi kutoka daraja la kwanza hadi la tano, kufuatia maboresho yanayowezesha ndege kubwa aina ya Bombardier Q400 yenye uwezo wa kubeba abiria 74 kutua kwa usalama.
Msimamizi wa uwanja huo, Lugano Mwinuka, amesema hatua hiyo ni matokeo ya ukarabati mkubwa unaoendelea katika uwanja huo ulioko Kata ya Ibadakuli, Manispaa ya Shinyanga, ambao umefikia zaidi ya asilimia 90 ya ukamilishaji.
“Kukamilika kwa mradi huu kutafanya ndege aina ya Bombardier Q400 ziweze kutua kwa urahisi, jambo linalokipandisha hadhi kiwanja kutoka daraja la kwanza hadi la tano katika viwango vya zimamoto na usalama wa anga,” amesema Mwinuka leo Oktoba 17, 2025 wakati wa ziara ya mkuu wa mkoa huo.
Ameeleza kuwa kazi kubwa zilizobaki ni za kiufundi na kiusalama, ikiwemo ukarabati wa njia ya kurukia na kutua ndege (runway), eneo la maegesho ya ndege, jengo la abiria, pamoja na maboresho ya mitaro ya maji, taa za usiku, uzio wa usalama na kituo cha hali ya hewa.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita (Mwenye gauni) akifanya ukaguzi wa jengo la abiria la uwanja wa ndege Shinyanga.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa TANROADS Mkoa wa Shinyanga, Chiando Mwinuka, amesema barabara kuu zote zinazounganisha uwanja huo na mikoa jirani kama Tabora na Mwanza tayari zimekamilika, hatua itakayorahisisha usafiri wa abiria na mizigo.
“Tumejenga barabara ya kisasa inayoingia moja kwa moja uwanjani, lengo ni kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo na kuongeza ufanisi wa huduma za anga katika mkoa wetu,” amesema Chiando.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema kukamilika kwa uwanja huo kutakuwa chachu ya mageuzi katika sekta za uchumi, biashara, utalii na usafiri wa anga, si kwa mkoa pekee bali kwa taifa kwa ujumla.
“Uwekezaji huu mkubwa utafungua milango kwa wafanyabiashara, wakulima na wawekezaji. Tumeuweka uwanja huu katika mpango wa kimkakati wa maendeleo ya mkoa ili kuunganisha fursa zilizopo na masoko mapya ndani na nje ya nchi,” amesema Mhita.
Ameongeza kuwa serikali ya mkoa inaendelea kuboresha mazingira rafiki kwa uwekezaji, hususan kwa kuzingatia uwepo wa kongani ya kitaifa ya kibiashara ya Buzwagi, ambayo inalenga kuchochea ukuaji wa uchumi wa ndani na kuongeza ajira kwa vijana.

Mradi huo wa upanuzi wa uwanja umegharimu Sh52 bilioni, ambapo asilimia 80 ya fedha zimetolewa na Benki ya Uwekezaji ya Umoja wa Ulaya (European Investment Bank), huku asilimia 20 zikigharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Kukamilika, kiwanja hicho kinatarajiwa kuwa miongoni mwa vituo muhimu vya anga Kanda ya Ziwa, kikichochea biashara, uwekezaji na maendeleo ya kijamii katika mikoa ya jirani.