
Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kusini, Aden Mayala amekihama chama hicho na kuhamia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Mayala ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amehama leo Jumatano Oktoba 22, 2025 mbele ya Rais na mgombea wa urais wa CCM, Samia Suluhu Hassan, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Kecha, Kinyerezi wilayani Ilala jijini Dar es Salaam.
Aden amepokewa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Asha- Rose Migiro mbele ya mgombea urais wa chama hicho.
Mwenyekiti huyo amekihama chama hicho ikiwa zimepita siku 10 tangu aliyekuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria, Ezekiah Wenje kukihama chama hicho na kuhamia CCM.
Wenje ambaye pia ni mbunge wa zamani wa Nyamagana kwa tiketi ya Chadema, alikihama chama hicho Oktoba 13, 2025 katika mkutano wa kampeni uliofanyika eneo la Chato mkoani Geita.