
Dar es Salaam. Kutokana na wimbi la mastaa wa kike kuzidi kujiingiza kwenye biashara ya vyakula maarufu ‘mama lishe’, staa wa muziki na mjasiriamali Bongo, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ameibuka na kusema yeye ndio role model wao kwani ndiye aliyeanza kabla ya wote.
Akipiga stori na Mwananchi, Shilole amesema anafurahi kuona kile alichoanzisha kinaigwa na wasanii wenzake wengi ila tahadhari ni kwamba wanatakiwa kukomaa sana kwani vitu vya kuiga bila kuwa na misingi imara vitawasumbua.
“Iko hivi, kuiga kitu sio vibaya ila mbaya kuiga kitu kibaya, sasa naona baadhi ya mastaa wengi wameibuka kuanzisha mama lishe kama ninavyofanya mimi, niseme tu sawa wameniiga wengi lakini wanatakiwa kuwa na misingi imara vinginevyo wataanguka.
“Nimekuwa mfano wa kuigwa kwa sababu mimi ndiye niliyekuwa wa kwanza kuanzisha mama lishe kwa kufungua mgahawa ndiyo wengine wakafuata hivyo watambue kuwa aliyeanza kaanza tu, niko kwenye biashara hii kwa muda mrefu hivyo naamini hakuna wa kunishinda,” amesema Shilole.
Shilole ameanza biashara ya mama lishe tangu mwaka 2014 na alianza na jina la Chuna Buzi ambalo alilitoa kwenye wimbo wake na baadaye akaja kubadilisha jina na kuita Shishi Food. Hadi sasa migahawa yake iko jijini Dar es Salaam na Dodoma.
Wasanii wengine kama Eshe Buheti ni maarufu kwa mapishi pia na aliwahi kuwa na majibizano na Shishi kuhusu nani mkali wa mapishi kati yao.