
Dar es Salaam. Msanii mkongwe wa Bongofleva, Chid Benz, amesema kutokana na kupitia changamoto za utumiaji wa dawa za kulevya na kuweza kuachana nazo, ana mpango wa kufanya dua maalum ili kujiondolea mikosi.
Chid Benz ameliambia Mwananchi kuwa, anaona mapito aliyopitia sio kitu cha kawaida kwa hiyo anataka kumuomba Mungu amuepushe na majanga kama hayo ya kimaisha ili aweze kuimarika zaidi.
“Kilikuwa kipindi kigumu kwangu, nimepitia kwenye changamoto za mfululizo lakini namshukuru Mungu nipo imara kwasasa, nitafanya maombi maalum ya kumshukuru Mungu ili aniepushe nisiweze kurudi tena huko,” amesema Chid.
Staa huyo wa Hip Hop ambaye jina lake halisi ni Rashid Makwiro, pia aliishukuru Serikali kupitia DCEA, Basata pamoja na Watanzania wote waliokuwa wakimuombea kwa kipindi chote alichokuwa akipatiwa matibabu, na kuongeza kuwa kwa matibabu aliyoyapata hivi karibuni hawezi kurudia matumizi ya dawa za kulevya na anaendelea kufanya shughuli zake za muziki kama kawaida.
Msanii huyo ambaye amewahi kutamba na nyimbo kama Dar es Salaam Stand up, Mashallah, Popompoo na nyingine, hivi karibuni ameonekana afya yake kuimarika na kuwa kivutio kwa mashabiki.