Milan, Italia. Mchezaji nyota wa Napoli, Kevin De Bruyne, alionekana kushindwa kujizuia kwa hisia baada ya kuipa timu yake bao la kuongoza kupitia mkwaju wa penalti, lakini akajiumiza wakati wa kupiga shuti hilo.

Kikosi cha Antonio Conte kilikuwa kinamenyana na Inter Milan Jumamosi jioni katika mchezo muhimu wa kuwania usukani wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A), huku timu zote mbili zikiwa na pointi 15 kabla ya mpira kuanza.

Baada ya dakika zaidi ya thelathini za mchezo, Napoli walipata nafasi ya kwanza ya kufunga kupitia penalti baada ya mchezaji wao kuchezewa vibaya ndani ya boksi la Inter.

Mchezaji huyo wa zamani wa Manchester City alionesha utulivu mkubwa alipokaribia kuchukua mkwaju huo na kuiweka Napoli kifua mbele.

Hata hivyo, alipokuwa akisherehekea bao hilo, De Bruyne mwenye umri wa miaka 34 ghafla alikumbwa na maumivu, akishika misuli ya nyuma ya paja lake.

Wachezaji wenzake walimzunguka kwa haraka, wakiwa hawaamini kilichotokea, huku mwenyewe akionekana akitoa machozi.

Madaktari wa Napoli waliingia haraka uwanjani, lakini badala ya kumtibu papo hapo, walimsaidia kutoka nje ya uwanja mara moja.

Baadaye, alionekana amekaa kwenye benchi akiwa amefungwa bandeji nene katika sehemu iliyoumia, akiangalia wenzake wakimaliza kazi kwa ushindi wa 3-1, ambao uliwaweka kileleni mwa Serie A.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *