Majadiliano yamefanyika katika Jukwaa la Suluhisho la Doha kwa Maendeleo ya Kijamii na katika mkutano wa kwanza wa viongozi wa Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Umaskini, uliofanyika kandokando ya Mkutano wa Pili wa Dunia kuhusu Maendeleo ya Kijamii unaoanza rasmi kesho Jumanne.
Kujifunza kutoka kwa kila mmoja
Akifungua Jukwaa la Suluhisho, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock amesema tukio hilo linaashiria mabadiliko ya makusudi kutoka “kukodolea macho tatizo” hadi kuchukua hatua kwa kutumia njia zilizothibitishwa.
“Mara nyingi tunakabiliwa na hali ambapo hatuna suluhisho dhahiri, hakuna jibu kwa mateso tunayoyaona, na hilo huvunja moyo. Au tuna suluhisho, lakini hatuwezi au hatutaki kufanya kile kinachopaswa kufanywa, jambo linalovunja moyo zaidi.”
“Leo ni tofauti: tuko hapa kuepuka mitego hiyo,” ameongeza, akisema kwamba, “kujifunza kutoka kwa kila mmoja; kunufaika na mawazo mazuri; kuunganisha nguvu; na kuishi kwa kufuata misingi yetu ya pamoja.”
Mifano dhahiri ya hatua mashinani
Tukio hilo, lililoandaliwa na Serikali ya Qatar kwa kushirikiana na Ufaransa na kuungwa mkono na Idara ya Masuala ya Kiuchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (DESA), lilikusanya pamoja maafisa wa serikali, wawakilishi wa sekta binafsi na wadau mbalimbali waliotoa mifano ya sera na miradi iliyofanikiwa katika nyanja kama vile kutokomeza umaskini, kazi zenye staha na ujumuishaji wa kijamii.
Bi. Baerbock ametoa mifano kutoka duniani kote, ikiwemo mpango nchini Sierra Leone unaowawezesha watu wenye ulemavu kupitia mafunzo, ajira, na mikopo midogo.
Nchini Sri Lanka, kituo cha ubunifu cha asasi za kiraia kinawafundisha vijana ujuzi wa ajira na kutumia mapato yaliyopatikana kuendeleza mafunzo zaidi, wakati nchini India mfumo wa kitaifa wa utambulisho wa kidijitali umewezesha kufunguliwa kwa zaidi ya akaunti milioni 300 za benki na kupanua upatikanaji wa huduma za kijamii.
Mikakati hii inaonyesha kinachowezekana pale ubunifu, ushirikiano na rasilimali zinapounganishwa, alisema, akihimiza wajumbe kuchukua fursa hizo.
Kuendeleza majawabu yanayoleta matokeo chanya
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Amina Mohammed amesisitiza umuhimu wa kusonga kutoka kwenye ahadi hadi utekelezaji. Kupitia ujumbe wake kwa njia ya video, amebainisha pia umuhimu wa Tamko la Kisiasa la Doha litakalopitishwa wakati wa Mkutano wa huo.
“Linataka mikataba ya kijamii inayowafaa watu – yenye haki, jumuishi na inayolingana na hali halisi za sasa,” amesema, akiongeza kwamba, “Ili kufanikisha hili, lazima tuendeleze suluhisho zinazofanya kazi,” aliwahimiza washiriki wajifunze kutoka kwa mifano iliyotolewa kwenye Jukwaa hilo.
“Tumieni simulizi hizi. Ziwachochee azma yenu. Pelekeni ujasiri huu kwenye jamii zenu na mgeuze kuwa vitendo vya kishujaa – leo na kwa vizazi vijavyo.”
Mhudumu wa afya akimpima mtoto kama kuna dalili za utapiamlo huko Khartoum, Sudan. Ulimwenguni kote, migogoro na mishtuko inayohusiana na hali ya hewa inasababisha njaa inayoongezeka, na kuacha familia zikijitahidi kupata chakula, matunzo na ustawi.
Muungano wa kimataifa wakutana kukabili janga la njaa
Mjadala wa kusaka majawabu umefanyika wakati viongozi walipokutana kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa ngazi ya juu wa Muungano wa Kimataifa Dhidi ya Njaa na Umaskini.
Zaidi ya watu milioni 670 wanakabiliwa na njaa na wengine bilioni 2.3 wanapata usalama mdogo au mkali wa chakula. Rais Baerbock amesisitiza kuwa janga la njaa la sasa si kwa sababu ya ukosefu wa chakula, bali “kutokana na ukosefu wa usawa, migogoro, na maamuzi ya kisera.”
“Hao ni mabilioni wanaojiuliza mlo wao unaofuata utatoka wapi,” amesema, akiongeza kuwa, “Wazazi wakitazama watoto wao wakilala njaa… janga la njaa si ukosefu wa chakula. Linaweza kuzuilika kabisa.”
Dunia inapopata joto, hali ya kutokuwa salama inaenea
Ameelezea hasa mabadiliko ya tabianchi kama kichocheo kinachoendelea kwa kasi cha ukosefu wa chakula.
Akitaja ardhi za kilimo za Sahel zilizogeuka kuwa vumbi, amesema hilo ni “eneo jipya la linaloongoza kwa ukosefu wa chakula,” akionya kuwa ongezeko la joto duniani lisipodhibitiwa linaweza kusukuma hadi watu bilioni 1.8 zaidi katika njaa.
Muungano wa Kimataifa – uliozinduliwa chini ya Uenyekiti wa G20 wa Brazil mwaka 2024 – sasa una wanachama takribani 200, wakiwemo serikali za kitaifa, mashirika ya kikanda, taasisi za kimataifa na makundi ya kiraia.
Mkutano wa Jumatatu umelenga kuimarisha hatua za pamoja, ikiwa ni pamoja na kupanua ulinzi wa kijamii, kusaidia riziki vijijini na kuwekeza katika kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabianchi.
“Katika dunia yenye wingi wa chakula – ambapo kunapaswa kuwa na vyakula vya kutosha kwa kila mtu – kuhakikisha kila mtu, kila mahali, anapata chakula cha kutosha inawezekana kabisa,” amesema Bi. Baerbock.
“Dunia isiyo na njaa na umaskini si ndoto ya mbali. Iko karibu, ikiwa tutajitahidi pamoja kuifikia,” amesema.
Habari za Umoja wa Mataifa kutoka Doha
Idhaa ya Umoja wa Mataifa iko Doha, ikikuletea taarifa wiki nzima, yakiwemo mahojiano na uchambuzi kutoka Mkutano huo. Fuata taarifa zetu hapa.