Kupitishwa kwa azimio hilo ni ahadi ya pamoja ya serikali kukabiliana na umasikini, kuunda ajira zenye staha, kupinga ubaguzi, kupanua upatikanaji wa ulinzi wa kijamii na kulinda haki za binadamu. Pia linatambua kuwa maendeleo ya kijamii si wajibu wa kimaadili pekee, bali ni sharti muhimu kwa amani, uthabiti na ukuaji endelevu.
Mkutano huo umehudhuriwa na zaidi ya wakuu wa nchi na serikali 40, idadi ya mawaziri 170, wakuu wa mashirika ya kimataifa, viongozi wa vijana, asasi za kiraia na wataalamu – zaidi ya wadau 14,000 wakiwa wamekusanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kitaifa cha Qatar. Mandhari ya mkutano imeonesha wazi kuwa maendeleo ya kijamii ni jukumu la wote, si serikali pekee.
Azimio la Doha lalenga kuimarisha maendeleo jumuishi na endelevu
Washiriki wa WSSD wakijumuika katika moja ya maeneo ya kutangamana kwenye mkutano huo.
Azimio hili, lililopewa jina la mji wa Doha ambako limepitishwa, linaimarisha tena dhamira ya viongozi kwa Azimio la Copenhagen la mnamo mwaka 1995 na Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu. Limejikita katika nguzo tatu kuu zinazounganisha maendeleo ya kijamii: kutokomeza umasikini, ajira kamili na yenye tija kwa wote, na ujumuishaji wa kijamii.
Azimio linaunganisha haki ya kijamii na amani, usalama na haki za binadamu, likiahidi “kutomwacha mtu nyuma.” Pia limetoa wito wa kuchukua hatua za haraka za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi chini ya Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC) na Mkataba wa Paris, likirejelea kanuni za Azimio la Rio, ikiwemo wajibu wa pamoja lakini unaotofautiana kulingana na uwezo wa kila nchi.
Ufadhili umepewa kipaumbele: azimio linauthibitishia tena Ajenda ya Addis Ababa kuhusu Ufadhili wa Maendeleo, huku likikaribisha Ahadi ya Sevilla ya kurekebisha mfumo wa ufadhili, na linataka taasisi za kimataifa ziwe zenye uwakilishi mpana na usawa zaidi.
Utekelezaji wa azimio utafuatiliwa na Tume ya Maendeleo ya Kijamii, kupitia mchakato wa mapitio kila baada ya muda wa miaka mitano ili kupima maendeleo na kuziba mapengo.
Wito wa kuhakikisha hakuna anayeachwa nyuma
Akizungumza baada ya kupitishwa kwa azimio hilo, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, amesema Doha lazima “ifikishe juhudi hizi ukingoni” kwa kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
Akitafakari maendeleo tangu Copenhagen, amebainisha kuwa ukosefu wa ajira umepungua duniani na umasikini uliokithiri umeshuka, lakini tofauti kubwa bado zipo, hasa kwa wanawake na vijana. Ameonya kuwa ukuaji wa uchumi pekee haujatosha kushughulikia ukosefu wa usawa wa kimfumo, akisisitiza kuwa mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la watu na migogoro vinaongeza udhaifu wa kijamii.
Bi. Baerbock ametoa wito wa suluhisho jumuishi linalounganisha mapambano dhidi ya umasikini, njaa, elimu duni, huduma za afya, usawa wa kijinsia na uhimilivu wa tabianchi, akisisitiza kuwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) “si malengo 17 yaliyotengwa, bali mfumo mmoja unaoendeleza maendeleo katika nyanja zote.”
“Haya si ajenda zilizotengwa — zote zinaonesha kuwa usalama wa binadamu ndio msingi wa usalama wa dunia,” amesema.
Washiriki kwenye mkutano wa pili wa Maendeleo ya Kijamii, WSSD, Doha, Qatar
Guterres: Azimio la Doha ni ‘chanjo ya uhai’ kwa maendeleo
Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kuwa kasi ya utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ni ndogo mno, huku malengo mengi yakiwa yamesimama au kurudi nyuma.
“Azimio la Kisiasa la Doha ni kama chanjo ya uhai kwa maendeleo,” amesema, akilielezea kama “mpango wa watu” unaolenga kupanua ulinzi wa kijamii kwa wote, kuhakikisha upatikanaji sawa wa elimu na afya, kuunda ajira zenye staha, na kuziba pengo la kidijitali.
Amesisitiza pia umuhimu wa mageuzi katika mfumo wa kifedha wa kimataifa ili kuhakikisha upatikanaji wa haki wa fedha za maendeleo na za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, hasa kwa nchi zinazoendelea zinazokabiliwa na mzigo wa madeni.
Akihitimisha, Katibu Mkuu amesema mkutano huu ni “wa matumaini kupitia hatua za pamoja” – na ni kuhusu kuamsha nia ya kisiasa na kifedha ili kutimiza ahadi iliyotolewa tangu Copenhagen.
“Tukiongozwa na Azimio la Kisiasa la Doha, tutekeleze mpango huu shupavu wa watu — mpango ambao binadamu wanauhitaji na kuustahili,” amesema Guterres.