
Lengo kuu na faida za mpango huo
Kwa mujibu wa taarifa ya IOM iliyotolewa leo Dakar, mji mku wa Senegal, mpango huo— wa kwanza wa aina yake katika Afrika Magharibi — utatumia uzoefu wa muda mrefu wa IOM katika ukusanyaji wa takwimu kuhusu wahamiaji waliopotea na usimamizi wa uhamiaji, ili kuimarisha uratibu wa kitaifa kuhusu suala hili katika nchi hizo mbili. Mradi huo unalenga kuhakikisha ushirikiano wa taasisi zote za serikali katika kukabiliana na changamoto zinazojitokeza pale wahamiaji wanapopotea au kufariki dunia.
“Kwa kuwezesha serikali za kitaifa na za mitaa, na kuimarisha ushirikiano wa kuvuka mipaka, tunasaidia kuokoa maisha, na pia kurejesha matumaini na heshima kwa familia ambazo zimekuwa zikisubiri majibu kwa muda mrefu,” amesema Sylvia Ekra, Mkurugenzi wa IOM kwa Kanda ya Afrika Magharibi na Kati.
Amesema “uongozi wa Gambia na Mauritania katika suala hili unaweka mfano mpya wa jinsi hatua za pamoja za kitaifa zinavyoweza kukabiliana ipasavyo na changamoto hii ngumu.”
Wimbi la vifo na hatari zinazowakumba wahamiaji
Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, IOM imeorodhesha idadi ya vifo zaidi ya 30,000 vya wahamiaji katika Bahari ya Mediterania, vifo 5,000 katika njia ya Atlantiki Magharibi kuelekea Hispania, na takribani vifo 6,000 katika jangwa la Sahara.
Tukio la hivi karibuni la kuzama kwa boti mnamo mwezi Agosti mwaka huu 2025 karibu na mji mkuu wa Mauritania, Nouakchott, lililosababisha vifo vya takribani watu 134, limeonesha dhahiri umuhimu wa kuchukua hatua.
Ahadi na hatua za serikali shiriki
“Kukabiliana na changamoto ya wahamiaji wanaopotea ni kipaumbele muhimu kwa Serikali ya Gambia,” amesema Sering Modou Njie, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Kimataifa na Wagambia Wanaoishi Ughaibuni.
Ameongeza kuwa, “lengo letu ni kuzuia vifo na kupotea kwa wahamiaji, huku tukihakikisha familia zinapata majibu na utulivu wanaostahili. Mradi huu unakuja wakati muafaka, tukiwa tumekamilisha uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Wapotevu na kuimarisha ushirikiano na nchi jirani ili kukabiliana kwa pamoja na changamoto hii.”
Kupitia mpango huu, Gambia na Mauritania zitaanzisha mifumo ya serikali yenye uratibu mzuri kwa ajili ya kuchunguza kesi za wahamiaji waliopotea, kubaini utambulisho wa waliopoteza maisha, na kuwapatia familia taarifa na majibu wanayostahili.
Mafunzo maalum na ushauri elekezi vitatolewa ili kuimarisha uwezo wa taasisi na ushirikiano wa mipakani, hivyo kuwezesha nchi hizi kuwatafuta waliopotea, kutambua miili ya marehemu na kuzuia matukio haya kusahauliwa.
Fatma Mohamed Salem, Mkurugenzi wa Mipaka, Wakimbizi na Masuala ya Uhamiaji katika Wizara ya Mambo ya Ndani na Uendelezaji wa Serikali za Mitaa, Mauritania, amesema, “njia ya bahari ya Atlantiki upande wa Afrika Magharibi bado inaendelea kusababisha majanga ya kibinadamu. Kupitia mradi huu, tunalenga kuonesha wazi juu ya wale waliopoteza maisha, kusaidia familia kupata majibu, na kuimarisha juhudi za kuzuia matukio kama haya.”
Ushirikiano wa kimataifa na njia za utekelezaji
IOM itatekeleza mradi huu kwa kushirikiana na Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC), Timu ya Argentina ya Anthropolojia ya Uchunguzi wa Vifo (EAAF), na Mashirika ya Kitaifa ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu, katika maeneo ya utambuzi wa miili, ufuatiliaji wa familia na msaada wa kisaikolojia.
Hatua ya IOM kuelekea suluhisho endelevu
Mpango huu ni sehemu ya juhudi za IOM za kusonga mbele zaidi ya ukusanyaji wa takwimu pekee kuhusu wahamiaji waliopotea — kuelekea kwenye utekelezaji wa vitendo vinavyolenga kuhakikisha familia zinapata majibu, faraja na msaada, huku nchi wanachama zikisaidiwa kukabiliana kwa ufanisi na changamoto hii ya dharura.