Dar es Salaam. Yanga na Simba zimepata ratiba rafiki ya hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu baada ya kupangwa kuanzia mechi zao nyumbani na kisha kumalizia nyumbani.

Timu hizo ambazo zimepanga kuutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam kwa mechi zao za nyumbani, zimepata fursa hiyo kwa vile kile moja ilikuwa katika chungu cha pili kwenye upangaji wa droo ya hatua hiyi, jana Jumatatu, Oktoba 3, 2025 huko Johannesburg, Afrika Kusini.

Yanga katika droo hiyo imepangwa katika kundi B ambalo litakuwa na timu za Al Ahly, AS FAR na JS Kabylie.

Simba imepangwa kundi D na timu za Esperance, Petro de Luanda na Stade Malien.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Yanga itaanzia nyumbani dhidi ya AS FAR ya Morocco kisha mchezo utakaofuata itakuwa ugenini dhidi JS Kabylie ya Algeria.

Mechi ya tatu kwa Yanga itakuwa ya ugenini dhidi ya Al Ahly na mechi ya nne, Yanga itakuwa mwenyeji wa Al Ahly ya Misri.

Baada ya hapo itasafiri hadi Morocco kucheza na AS FAR na mechi ya mwisho itakuwa nyumbani dhidi ya JS Kabylie.

Simba itaanza nyumbani kwa kuikabili Petro de Luanda ya Angola na mchezo utakaofuata itaenda Mali kucheza na Stade Malien.

Baada ya hapo, Simba itaenda kucheza Tunisia na Esperance na zitarudiana hapa Dar es Salaam katika mechi ya nne.

Simba katika mechi ya tano itakuwa ugenini dhidi ya Petro de Luanda huko Angola na itamalizia nyumbani dhidi ya Stade Malien.

Katika Kombr la Shirikisho, kitendo cha wawakilishi wawili wa Tanzania, Singida Black Stars kuwekwa katika chungu cha nne kwenye uchezeshaji wa droo, kimewafanya wajikute wakianzia ugenini na kumalizia ugenini.

Azam imepangwa katika kundi B ambalo litakuwa na timu za Wydad AC, Maniema Union na Nairobi United.

Azam itaanzia DR Congo kucheza na Maniema Union na baada ya hapo itakuwa nyumbani kucheza na Wydad AC ya Morocco.

Mchezo wa tatu itakuwa ugenini kucheza na Nairobi United huko Kenya na kisha zitarudiana hapa Tanzania kwa mechi ya nne.

Mechi ya tano itakuwa hapa Tanzania dhidi ya Maniema Union na itamalizia huko Morocco dhidi ya Wydad AC.

Singida Black Stars ambayo ipo kundi C, itaanzia ugenini kucheza na CR Belouizdad ya Algeria na mchezo unaofuata itakuwa nyumbani dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini.

Mechi ya tatu itakuwa nyumbani kucheza na AS Otoho ya Congo kisha zitarudiana hapa nchini katika mechi ya nne.

Singida BS itakuwa nyumbani kucheza na CR Belouizdad katika mechi ya tano na itafunga hesabu kwa kucheza na Stellenbosch huko Afrika Kusini.

Mechi za kwanza za hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika msimu huu zitachezwa kati ya Novemba 21 hadi 23 mwaka huu na za pili zitachezwa kati ya Novemba 28 hadi 30.

Mechi za tatu zitachezwa Januari 23 hadi 25, 2025 na za nne zitachezwa kuanzia Januari 30 hadi Februari  Mosi, 2026.

Mzunguko wa tano wa hatua ya makundi utakuwa kuanzia Februari 6 hadi 8, 2026 na mechi za kufunga hatua ya makundi zitachezwa kati ya Ferbruari 13 hadi 15, mwakani.

MAKUNDI LIGI YA MABINGWA AFRIKA

RS Berkane (Morocco)

Pyramids FC (Misri)

Rivers United (Nigeria)

Power Dynamos (Zambia)

Al Ahly (Misri)

Yanga (Tanzania)

AS FAR (Morocco)

JS Kabylie (Ageria)

Mamelodi Sundowns (Afrika Kusini)

Al Hilal (Sudan)

MC Alger (Algeria)

Saint-Eloi Lupopo (DR Congo)

Esperance (Tunisia)

Simba (Tanzania)

Petro de Luanda (Angola)

Stade Malien (Mali)

MAKUNDI KOMBE LA SHIRIKISHO AFRIKA

USM Alger (Algeria)

Djoliba (Mali)

Olympic Safi (Morocco)

San Pedro (Ivory Coast)

Wydad AC (Morocco)

Maniema Union (DR Congo)

Azam FC (Tanzania)

Nairobi United (Kenya)

CR Belouizdad (Algeria)

Stellenbosch (Afrika Kusini)

AS Otoho (Congo)

Singida Black Stars (Tanzania)

Zamalek (Misri)

Al Masry (Misri)

Kaizer Chiefs (Afrika Kusini)

Zesco United (Zambia)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *