Nyota wa soka wa Ureno, Cristiano Ronaldo, ameibuka tena na kuishambulia Manchester United, akidai kuwa kocha Ruben Amorim hawezi kufanikiwa klabuni hapo kwa sababu ya muundo dhaifu ndani ya timu hiyo.

Ronaldo, ambaye aliondoka United mwaka 2022 baada ya mahojiano mazito na mtangazaji Piers Morgan, amesema matatizo yaliyokuwa yakiiandama klabu hiyo bado yapo hadi leo.

“Ninajisikia huzuni kwa sababu Manchester United ni moja ya klabu kubwa duniani, na klabu ambayo bado ipo moyoni mwangu kwa sababu nyingi.

“Unatakiwa kuwa na watu wenye akili na mipango mizuri ili kuunda msingi wa baadaye. Hapo zamani United walikuwa na akina Nicky Butt, Gary Neville, Roy Keane, Beckham wote walikulia klabuni na wakawa mastaa wakubwa. Lakini kwa sasa, Manchester United haina muundo wowote thabiti,” amesema Ronaldo katika mahojiano na Morgan.

Ronaldo alisisitiza kuwa bado ana matumaini hali hiyo itabadilika siku zijazo, akisema uwezo wa klabu hiyo ni mkubwa lakini viongozi wamekuwa wakikosa mwelekeo.

“Amorim hawezi kufanya miujiza”

Kuhusu kocha Ruben Amorim, ambaye amekuwa chini ya shinikizo kutokana na mwanzo mbaya wa msimu, Ronaldo alimkingia kifua lakini pia akaweka wazi hali halisi.

“Anajaribu kadri ya uwezo wake. Lakini miujiza haiwezekani, Kama tunavyosema Ureno, miujiza ipo Fatima pekee! Amorim hawezi kufanya miujiza. Wana wachezaji wazuri, lakini baadhi yao hawajui maana ya kuvaa jezi ya Manchester United.” amesema staa huyo wa Al-Nassr.

Amorim ameiongoza United kutopoteza katika mechi nne mfululizo za Ligi Kuu England, ikiwemo sare ya 2-2 dhidi ya Nottingham Forest, lakini bado wanakosolewa kwa mwenendo wa uchezaji.

“Manchester bado ipo moyoni mwangu”

Ronaldo, aliyefunga mabao 145 katika mechi 346 alizoichezea United, alisema ni maumivu makubwa kuona klabu hiyo ikizidi kuyumba.

“Bila shaka inauma. Nilicheza hapo miaka mingi, nikashinda Ligi ya Mabingwa, Ballon d’Or, na mataji zaidi ya 12.

Manchester United bado ipo moyoni mwangu. Lakini tukubaliane ukweli hawapo kwenye njia sahihi. Tatizo si kocha peke yake, bali ni mfumo mzima wa klabu,” amesema.

Kwa maneno yake hayo, Ronaldo ameibua mjadala mpya kuhusu mustakabali wa Amorim na namna ambavyo uongozi wa United unavyoshughulikia changamoto za klabu hiyo kongwe ya Old Trafford.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *