Wafanyabiashara wanaelezea kuwa si nia yao kuwatia hasara wateja wao wanaosafiri hata kutoka mataifa jirani.
Wanasema kumekuwa na kile walichokiita kunyanyaswa na walimili wa majengo wanayotumia kwa biashara pamoja na kodi za juu wanazotozwa na mamlaka ya Mapato.
Wateja wengi kutoka ndani na nje ya Uganda hupata hasara kubwa kutokana na migomo hii ya kila mara ya wafanyabiashara hasa wa jumla katikati mwa mji wa Kampala.
Wanapofanya safari kutoka sehemu mbalimbali za Uganda na hata mataifa jirani, wateja hao ambao wengi wao ni wafanyabiashara wa rejareja hukumbana na hali ambapo maduka ya bidhaa walizokwenda kununua yamefungwa kutokana na migomo hiyo.
Hii huwatia katika hasara ya kukodi mahala pa kulala kusubiri maduka hayo yafunguliwe au kukata tama na kurudi makwao. Mmoja kati ya wateja Cerina Nagujja hatua hiyo imeleta usumbufu kwa wateja.
Kwa upande wao, wafanyabiashara wanalalamikia tabia za wenye majengo kupandisha kodi kila mara na pia kwa masharti kwamba anayekosa kulipa kabla ya kuanza mwezi mpya haruhusiwi kufungua duka lake.
Tozo nyingine wanazotakiwa kutoa wenye maduka kama vile kulipia ukusanyaji taka na kusafisha, maji na umeme nazo zinaelezewa kuwa za juu.
Mfanyabiashara mmoja ambaye aliomba kutotajwa jina amesema kila upande unategemeana katika kuhakikisha uchumi wa nchi unakuwa.
Lakini malalamiko jumuishi ya wafanyabiashara ni ushuru mkubwa wanaotozwa kwa bidhaa wanazoagiza kutoka nje ya nchi.
Hivi karibuni, mamlaka ya mapato imepandisha kodi kwa bidhaa za nguo kama hatua ya kuwalazimu wafanyabiashara kuondokana na kuagiza nguo kutoka nje ya nchi ili zile zinazotengenezwa nchini zipate soko.
Wageni kuingia katika biashara za wenyeji
Lakini wafanyabiashara wanaelezea kuwa nguo kutoka kwenye viwanda vya nchini ni za bei ya juu na watu wengi hawawezi kuzinunua. Isitoshe viwanda hivyo vinamilikiwa na wawekezaji kutoka China ambao kwa namna nyingine huleta nguo zilizokwisha kushonwa kwa hiyo ushindani kati yao na wenyeji wafanyabiashara huonekana kuwapendelea wawekezaji hao. Issa Sekito ni msemaji wa shirikisho la wafanyabiashara KACITA
“Tumekuwa tumelalamika juu ya uwepo wa wachina katika biashara za rejareja, lakini hakuna majibu kutoka kwa serikali, ikiwa haya malalamiko hayatashughulikiwa tutayafunga maduka.”
Mwanzoni mwa wiki wafanyabiashara wengi katikati ya jiji walipata hasara kubwa kufuatia mafuriko yaliharibu bidhaa zao.
Chanzo cha mafuriko hayo ilikuwa kuziba kwa mtaro wa majitaka uliozibwa na mwekezaji mmoja ambaye anaendesha mradi wa ujenzi wa maduka juu yake.
Ijapokuwa serikali imeahidi kuwafidia, wafanyabiashara wanasisitiza kuwa mradi huo utaendelea kusababisha mafuriko yanayoweza kuepukika.