
Rais Paul Biya anaapishwa leo Alhamisi, Novemba 6, kwa muhula wake wa nane wa urais. Huu ni utaratibu tu kwa mtu aliyeapishwa kwa mara ya kwanza Novemba 6, 1982, miaka 43 iliyopita hadi leo. Tarehe hii inaashiria kuingia kwake madarakani. Sherehe hiyo inaoekana kuwa ya heshima na ya kifahari, licha ya mvutano mkali wa baada ya uchaguzi.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Huko Yaoundé, nchini Cameroon, maandalizi yanaendelea. Kama inavyoripotiwa na mwandishi wetu Polycarpe Essomba, mji mkuu umepambwa kwa ajili ya sherehe kubwa: sanamu za mkuu wa nchi katika kila makutano na mabango yanayoonyesha ujumbe ulioandikwa kwa Kifanransa na Kingereza “Asante kwa raia wazalendo kwa nchi yao walionichagua”.
Kwa upande wa sherehe, Bunge la taifa, ambalo linaandaa hafla hiyo, limepania kufanya sherehe hii kuwa kubwa zaidi. Mialiko isiyopungua 1,500 ilitumwa kwa viongozi wa nchi na mabalozi wa nchi za kigeni nchini Cameroon. Wakati huu, mabalozi wa nchi za Magharibi—kutoka Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake, Marekani, Uingereza, na Canada—wote wamealikwa, ingawa hawakuwapo wakati matokeo ya uchaguzi yalipotangazwa katika Baraza la Katiba.
Wagombea walioshindwa pia wamepokea mialiko, akiwemo Issa Tchiroma Bakary, ambaye anaendelea kudai ushindi katika uchaguzi wa Oktoba 12 na anasema amejificha.
Hotuba inayosubiriwa kwa hamu baada ya miezi kadhaa ya ukimya
Sherehe inatarajia kuanza kwenye saa sita mchana saa za huko, na kuwasili kwa rais Paul Biya na mkewe katika jengo la Bunge la taifa. Baada ya kula kiapo, Paul Biya atatoa hotuba inayotarajiwa sana: hii itakuwa taarifa yake ya kwanza kwa umma tangu kuanza kwa mchakato wa uchaguzi.
Anapoanza muhula huu mpya, mkuu wa nchi anatarajiwa kuelezea mwelekeo anaokusudia kuchukua kwa nchi, kufuatia uchaguzi uliojaa vurugu, vifo, na watu kukamatwa. Wengi wanatumai ujumbe wa kutuliza na matangazo makali yanayoelekezwa kwa wale wanaopinga kuchaguliwa kwake tena – iwe ni viongozi wa kisiasa au vijana ambao wameingia mitaani katika siku za hivi karibuni.