Sekta ya chai nchini imeende­lea kuwa miongoni mwa nguzo muhimu za uchumi, ikichangia ajira, pato la Taifa na kuinua mai­sha ya maelfu ya wakulima vijijini. Lakini pia chai ni mojawapo ya mazao ya biashara yanayoiingizia nchi fedha za kigeni.

Sekta hii imekuwa ikipata ngu­vu mpya miaka ya karibuni baada ya uboreshaji wa sera za uwekeza­ji, uboreshaji wa sekta ya kilimo, uwekezaji katika viwanda vya usindikaji na juhudi za kujenga soko la kimataifa lenye thamani zaidi.

Kilimo cha Chai ambacho awa­li ilikuwa ni shughuli ambayo wakulima wanaifanya kwa ajili ya kukidhi maisha yao ya kawaida, sasa ina fursa nyingi ikiwemo kuongeza thamani, kuunganisha wakulima wadogo kwenye min­yororo ya thamani ya zao hilo na kubore­sha uzalishaji kupi­tia teknolojia na miundombinu ya umwagiliaji.

Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bi. Beatrice Banzi

Hilo limesaid­ia kuongezeka kwa uzalishaji na thamani ya mauzo ya chai sokoni msimu wa hivi kari­buni. Serikali kupitia Bodi ya Chai Tanza­nia na wadau wamechukua hatua za kuwekeza katika kureje­sha viwanda vilivyokuwa ­wa vimeacha kuzalisha na kujenga vipya vya kuchakata ili kuongeza uwezo wa kusindika majani ya chai na kuzalisha “made tea” yenye ubora wa kuuza nje. Hatua hizi zimechangia kupanua soko la kuuza nje na kuongeza mapato ya sekta.

Katika mahojiano maalum na gazeti hili, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Chai Tanzania Bi. Beatrice Banzi alieleza maendeleo ya sek­ta hiyo, mafanikio yaliyopatikana chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, pamoja na mika­kati mipya inayolenga kuifanya chai ya Tanzania kuwa miongoni mwa chai bora zaidi duniani.

Sekta ya chai Tanzania na maendeleo yake

Bi. Beatrice anasema sekta ya chai Tanzania imepiga hatua kub­wa katika miaka ya hivi karibuni. Kwa sasa Tanzania inazalisha takribani tani 22,000 kwa mwaka lakini uwezo halisi wa kuzalisha ni tani 60,000 japokuwa kiasi kikub­wa (asilimia zaidi ya 90) kinaenda katika masoko ya nje kama Paki­stan, Japani, China, Qatar, Oman, UAE na kwingineko, jambo amba­lo linasababishwa na mwamko wa Watanzania katika matumizi ya chai na ukosefu wa elimu kuhusu umuhimu wa kinywaji hicho.

“Watanzania wengi hawa­na mwamko wa kutumia chai. Wengi wetu tunatumia chai kwa mazoea jambo ambalo sio sahi­hi kwani chai ni kinywaji chenye faida nyingi za kiafya mwilini iki­wemo kuboresha mzunguko wa damu, kukuepusha na magonjwa mbalimbali, kuupa mwili nguvu nk. Hivyo tunapaswa kutumia chai mara kwa mara kama tunavyo­tumia maji,” anasema Bi. Beatrice.

Anasema sekta ya chai imeku­wa ikiimarika kutokana na jitiha­da za Serikali, taasisi za utafiti, na mashirika ya maendeleo yali­yowekeza katika kuboresha mbe­gu, kuongeza tija na kuimarisha usimamizi wa ubora.

“Wakulima wetu wamean­za kuelewa thamani ya ubo­ra. Tunashuhudia ongezeko la matumizi ya mbegu bora na mbolea za kisasa, sambamba na elimu juu ya usimamizi bora wa mashamba. Lakini pia Seri­kali imefanya kazi kubwa katika kutoa ruzuku ya pembejeo za kili­mo ambazo zimekuwa msaada mkubwa kwa wakulima,” anaele­za Bi. Beatrice.

Juhudi za Serikali kufungua fursa za masoko na uwekezaji

Akizungumzia mchango wa Serikali ya Awamu ya Sita chi­ni ya uongozi wa Rais wa Jam­huri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, Bi. Beatrice anasema kuwa Rais Samia ameleta mageuzi makub­wa katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji.

“Rais Samia amekuwa kina­ra katika kufungua milango ya masoko mapya kupitia diploma­sia ya kiuchumi. Kupitia safari na mikutano yake na viongozi wa mataifa mbalimbali, chai ya Tanzania imepata mwanga mpya katika soko la dunia,” anasema Bi. Beatrice.

Anaongeza kuwa Serikali imewekeza pia katika miundom­binu ya barabara na umeme viji­jini, jambo lililosaidia kupunguza gharama za uzalishaji na usafir­ishaji wa chai kutoka mashamba­ni hadi viwandani.

“Uwekezaji wa Serikali katika miundombinu umeongeza ushin­dani wa wakulima wetu. Hii ni sehemu ya ajenda pana ya Rais Samia ya kufungua fursa za kiu­chumi vijijini,” anaeleza.

Anasema kupitia juhudi za Rais Samia katika kufungua milan­go, Bodi ya Chai imepata fursa ya kuhudhuria katika mataifa mbalimbali na kuonyesha nam­na chai ya Tanzania ilivyokuwa bora na hatua inayopitia katika uwekezaji wake.

“Ziara hizo zimetusaidia kufungua fursa mpya za masoko. Kwa mfano ziara tuliyoifanya Japan imewezesha wawekezaji wa Japan kufanya ziara maalu­mu nchini kwa ajili ya kuja kuona fursa zilizopo na wameshaanza mchakato wa kuwekeza kati­ka sekta ya chai,” anasema Bi. Beatrice.

Bodi ya Chai Tanzania: Kinara wa ukuzaji na uongezaji tija ya sekta ya chai

Bodi ya Chai Tanzania imekuwa kiungo muhimu kati ya wakulima, wazalishaji na soko. Bi. Beatrice anasema kuwa bodi hiyo imewe­ka mikakati ya kuimarisha uzal­ishaji kupitia mafunzo, utafiti, na uwekezaji katika teknolojia.

“Tumeanzisha mpango wa kitaifa wa kuongeza tija unaoju­muisha utoaji wa mafunzo kwa wakulima kuhusu kilimo bora cha chai, matumizi sahihi ya pembe­jeo na utunzaji wa mazingira. Pia tumeanzisha mashamba ya mfa­no,” anasema.

Kwa mujibu Bi. Beatrice hatua hizo zimeongeza uzalishaji kwa zaidi katika miaka mitatu iliyo­pita, huku ubora wa majani mab­ichi ukiongezeka kwa kiwango kikubwa. Mbali na hilo bodi pia imekuwa ikishirikiana na taasisi mbalimbali za Serikali na binaf­si katika kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua.

Mkulima akifurahia mavuno ya chai.

“Tumekuwa na ushirikia­no mzuri na taasisi mbalimbali hususani zilizpo chini ya Wizara ya Kilimo ikiwemo wakala wa mbegu, taasisi za utafiti wa kili­mo pamoja na nyingine chini ya Wizara ya Viwanda na Uwekezaji ikiwemo Tanzania Chamber of Commerce, Industry and Agri­culture (TCCIA), TANTRADE, TISEZA na KOTRA. Ushirikiano huu umesaidia kufungua fursa za masoko ya chai ndani na nje ya Tanzania,” anasema Bi. Beatrice.

Mnada wa Chai: Mkakati mpya wa kuboresha bei na kuongeza uwazi wa mauzo ya chai

Moja ya mafanikio makubwa ya sekta ya chai Tanzania ni kuan­zishwa kwa mnada wa chai jiji­ni Dar es Salaam mwaka 2023 ambao unaendeshwa na Bodi ya Chai Tanzania kwa kushirikiana na wadau kila siku ya Jumata­tu. Mnada huo unafanyika katika ghala la bodi hiyo lililopo eneo la Kipawa.

“Kabla ya hapo, chai nyingi za Tanzania ziliuzwa kupitia mna­da wa Mombasa. Hii ilipunguza udhibiti na uwazi kwa wazalisha­ji wetu. Lakini tangu tuanzishe mnada wetu, wakulima wamean­za kuona faida moja kwa moja,” anasema Bi. Beatrice.

Ameeleza kuwa mnada huo umeongeza ushindani na uwazi katika bei, ambapo wakulima sasa wanapata taarifa kamili kuhusu thamani ya zao lao sokoni.

“Kupitia mfumo wa kidijitali wa minada, bei zinatangazwa hadharani na wakulima wanawe­za kufuatilia mwenendo wa soko kwa wakati halisi. Hii imeonge­za imani, mapato na kuimarisha utendaji wa sekta kwa ujumla,” anaeleza Bi. Beatrice.

Ubora na thamani ya chai ya Tan­zania katika soko la dunia yapaa

Ubora wa chai ya Tanzania umeendelea kuvutia wanunuzi wa kimataifa. Bi. Beatrice anase­ma chai ya Tanzania ina ladha ya kipekee inayotambulika duniani.

Moja ya mashamba ya chai nchini likiwa katika muonekano wa kuvutia.

“Chai yetu ina harufu nzuri na ladha laini yenye asili ya udongo na mazingira ya asili ya kitan­zania. Hii ndiyo inayoifanya iwe tofauti na chai kutoka maeneo mengine,” anaeleza.

Anasema kuwa bodi imeen­delea kushirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) na mamlaka nyingine kuhakikisha viwango vya ubora vinafuatwa kuanzia shambani hadi sokoni.

“Kila mzigo wa chai unaopitia minadani na kusafirishwa nje hupimwa ubora wake. Tunataka chai ya Tanzania iwe nembo ya ubora Afrika Mashariki na duni­ani,” anasema Bi. Beatrice.

Anasema chai ya Tanzania sasa imekuwa na thamani kubwa kati­ka masoko mbalimbali duniani ambapo kwa wastani inauzwa kuanzia Dola za Marekani 1.55 hadi 60 kwa kilo kutegemeana na aina ya chai. Hili ni jambo la kujivunia kwani sisi ni moja ya nchi ambazo chai yetu ina ubora wa kipekee na thamani kubwa sokoni.

Uwekezaji katika teknolojia na mifumo ya kidijitali waongeza ufanisi wa sekta ya chai

Bodi ya Chai Tanzania imekuwa mstari wa mbele katika kutumia teknolojia kuboresha huduma zake. “Tumeanzisha mfumo wa kidijitali unaoruhusu wakulima kusajiliwa, kufuatilia uzalishaji wao na kupata taarifa kuhusu bei na masoko moja kwa moja kupi­tia njia za kidijitali,” anasema Bi. Beatrice.

Pia, bodi imeanza kutumia drones na GPS mapping katika kutambua maeneo ya uzalishaji na kuboresha takwimu za sekta.

“Teknolojia imetusaid­ia kuongeza uwazi na ufanisi. Tunaweza kufuatilia kila hatua ya uzalishaji na mauzo, jambo ambalo linasaidia kupanga mika­kati kwa uhalisia zaidi,” anaeleza.

Mikakati ya Bodi ya Chai katika miaka mitano ijayo

Akizungumzia dira ya bodi kwa miaka mitano ijayo, Bi. Beatrice anasema wanapanga kutekeleza mpango wa kitaifa wa kuinua sek­ta ya chai unaolenga kuongeza uzalishaji, thamani na ajira.

“Tumejipanga kuongeza uzal­ishaji wa chai kutoka tani 22,000 hadi kufikia zaidi ya tani 60,000 kwa mwaka. Lengo ni kuhakiki­sha Tanzania inakuwa miongoni mwa wazalishaji wakuu wa chai barani Afrika,” anasema.

Anasema wanataka kila mkoa unaolima chai uwe na kiwanda chake, jambo ambalo litapunguza gharama za usafiri na kuonge­za thamani kwa wakulima. Pia wakulima wadogo watapewa nafasi ya kumiliki viwanda vido­go vya usindikaji kupitia ushirika. Hii ni hatua ya kuongeza kipato chao na kuwapa umiliki zaidi wa mnyororo wa thamani.

Sekta ya chai Tanzania inakua kwa kasi, ikichochewa na sera thabiti za Serikali, ubunifu wa Bodi ya Chai na juhudi za wakuli­ma. Kupitia uwekezaji katika teknolojia, masoko, na usindika­ji, sekta hii ina nafasi kubwa ya kuwa injini ya maendeleo vijijini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *