
Jeshi la Israeli lilisema vikosi vyake viliyalenga maghala ya silaha kutoka kitengo cha juu cha Radwan cha wanamgambo hao wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran, vikilishutumu kundi hilo kwa kujipanga upya kinyume na makubaliano ya kusitisha mapigano.
Kabla ya mashambulizi hayo, jeshi la Israel IDF iliwataka wakazi kuondoka katika majengo fulani na mazingira yake katika maeneo matano kusini mwa nchi. Kulingana na shirika la habari la serikali NNA, Rais wa Lebanon Joseph Aoun alieleza mashambulizi hayo kama “uhalifu mkubwa” uliofanywa na Israeli.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa hapo jana waliyalaani mashambulizi hayo, wakiyaita kuwa ni ukiukwaji wa wazi wa azimio la Baraza la Usalama nambari 1701 na kuonya kwamba hatua za kijeshi “zinadhoofisha maendeleo yanayofanywa kuelekea suluhisho la kisiasa na kidiplomasia.
Taarifa kutoka kwa Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) ilisema iliitaka Israeli kusitisha mara moja mashambulizi haya na ukiukwaji wote wa azimio nambari 1701.