Waendesha mashtaka nchini Tanzania wamewafungulia mashtaka watu 98 kwa makosa ya uhaini, wakihusishwa na maandamano yenye vurugu yalioiibuka wakati wa uchaguzi wa wiki iliopita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Shirika la habari la Reuters limeweza kuona stakabadhi za mahakama zinazohusiana na kesi ya uhaini dhidi ya watu hao 98.
Chama kikuu cha upinzani Chadema pamoja na mashirika mengine ya kiraia yanasema walinda usalama nchini Tanzania walitekeleza mauaji ya zaidi ya watu Elfu moja.
Licha ya taarifa hiyo kutoka kwa upinzani na mashirika ya kutetea haki za binadamu, serikali ya Tanzania inasema takwimu hizo sio za kweli bila ya hata kuweka wazi idadi ya waliouawa.

Mashtaka haya ni ya kwanza dhidi ya watu wanaodaiwa kushiriki kwenye maandamano hayo ya wakati wa uchaguzi.
Kulingana na kiongozi mmoja wa kidini nchini Tanzania, hatua hii ya serikali inaweza kuchochea ghadhabu ya raia haswa wakati huu kukionekana kuwa na mgawanyiko kutokana na matokeo ya uchaguzi huo.
Viongozi wa kidini wametoa wito kwa serikali kujaribu kufanya mapatano na wapinzani wake wa kisiasa pamoja na waandamanaji.

Msemaji wa serikali ya Tanzania alikosa kujibu ujumbe wala simu za shirika la habari la Reuters kuhusuiana na kesi hii ya uhaini dhidi ya waandamanaji.
Waangalizi kutoka Umoja wa Afrika katika ripoti yao walisema kuwa uchaguzi wa Tanzania haukuwa wa huru na haki ambapo maofisa wake walithibitisha kujazwa kwa karatasi za kupiga kura kwenye masanduka ya kura siku ya uchaguzi kwenye baadhi ya vituo.