IOM Yasihi Suluhisho Endelevu kwa Wakimbizi wa Ndani Sudan Kusini

Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji la IOM, SungAh Lee, ametoa wito wa kuimarisha juhudi za kushughulikia hali ya wakimbizi wa ndani na wanaorejea makwao nchini Sudan Kusini, akisisitiza umuhimu wa suluhisho za kudumu zinazohakikisha usalama, utu na uthabiti kwa jamii zilizoathirika.

Taarifa kutoka Juba nchini Sudan Kusini na Geneva nchini USwisi imeeleza kuwa akiwa ziarani kwa wiki moja nchini Sudan Kusini, Lee alitembelea Malakal na Bentiu ambako alikutana na jamii zilizopoteza makazi kutokana na vita na mafuriko ya mara kwa mara. Alishuhudia pia juhudi za IOM katika kusaidia urejeaji na ujenzi upya wa maisha ya watu kupitia huduma za afya, chanjo, usafiri salama na msaada wa kijamii.

“Kile nilichokiona Sudan Kusini kinaonesha changamoto kubwa za wakimbizi wa ndani na uimara wa wananchi wanaojitahidi kujenga upya maisha yao,” alisema Bi. Lee. “Jamii hizi zinahitaji zaidi ya misaada ya dharura—wanahitaji fursa ya kurudi nyumbani salama, kuwapeleka watoto shule na kurejesha utu wao.”

Mlolongo wa madhila na ufinyu wa ufadhili

Sudan Kusini ni miongoni mwa nchi zilizoathiriwa zaidi na ukimbizi duniani, ikiwa na takribani watu milioni 9.3 wanaohitaji msaada wa kibinadamu, karibu milioni 2 wakiwa wakimbizi wa ndani, na zaidi ya milioni 1.3 waliokimbia mapigano nchini Sudan tangu Aprili 2023.

Kiongozi huyo wa IOM alikutana na maafisa wa serikali na mashirika ya Umoja wa Mataifa mjini Juba ili kuimarisha uratibu kati ya misaada ya kibinadamu na juhudi za maendeleo.

Ziara yake imekuja wakati mpango wa misaada ya kibinadamu ukiwa umefadhiliwa kwa asilimia 31 pekee, hali inayokwamisha utoaji wa msaada muhimu na maendeleo ya suluhisho za kudumu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *