KIKOSI cha Yanga, Jumapili ya Novemba 9, 2025 jioni, kimeshuka uwanjani kuumana na KMC katika mechi ya Ligi Kuu, huku kiungo mmoja mkabaji akipambana kulinda heshima aliyokuwa nayo tangu akicheza Uarabuni na sasa ni kama amerahisishiwa mambo pale Jangwani.

Kiungo huyo ni, Moussa Balla Conte ambaye kwa sasa ashindwe mwenyewe tu kutokana na taarifa za kiungo mwenzie Mudathir Yahya kutakiwa kuwa nje ajiuguze jeraha la goti.

Licha ya Mudathir kujumuishwa katika kikosi cha timu ya taifa iliyopo chini ya kaimu kocha mkuu, Miguel Gamond, inadaiwa kiungo huyo huenda akashindwa kujumuika na timu kwa vile ni majeruhi anasubiri majibu ya vipimo kama atafanyiwa upasuaji ama la.

Chanzo cha kuaminika kutoka Yanga ambacho hakikutaka jina liwekwe wazi, kimeiambia Mwanaspoti, Mudathir aliumia katika mechi dhidi ya Wiliete ya Angola akitumika kwa dakika 24 na hajarejea tena uwanjani hadi sasa.

CONT 01

“Tangu ameumia na Wiliete bado hajarudi na vipimo vya awali vimefanyika ana shida ya goti, majibu yatatolewa na daktari,” kimesema chanzo hicho na kuongeza;

“Inaelezwa majibu yatakapotoka ndiyo itafahamika kama ni kupata mapumziko ya muda kutokana na mechi za mara kwa mara ama kufanyiwa upasuaji kwani mchezaji mwenyewe analalamika ana maumivu makali.”

Kiungo huyo ambaye ni panga pangua kikosi cha kwanza cha Yanga chini ya makocha zaidi ya wanne waliopita kwa miaka ya karibuni akiwemo Nasreddine Nabi, Miguel Gamondi, Sead Ramovic na Miloud Hamdi.

Kukosekana Mudathir ni fursa kwa Conte ambaye licha ya kusajiliwa kwa mbwembwe, hajapata nafasi ya kuonyesha ufundi alionao mbele ya kiungo huyo na Duke Abuya ambao wamekuwa wakicheza pamoja mara kwa mara.

CONT 02

Katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu dhidi ya Mtibwa Sugar na Yanga kushinda mabao 2-0, eneo la kiungo mkabaji lilianza na Duke akisaidiana na Edmund John.

Mbali na Conte, pia kuna mchezaji mwingine ambaye pia ameonekana kuwa bora eneo la kiungo mkabaji, Aziz Andabwile ambaye alionyesha kuwa bora eneo hilo chini ya kocha Romain Folz aliyemalizana na Yanga hivi karibuni baada ya makubaliano ya pande mbili.

Conte amesajiliwa na Yanga akitokea CS Sfaxien ya Tunisia baada ya awali kutajwa kuhitajiwa na Simba, ambao walilazimika kwenda kumsajili Alassane Kante ambaye ameonekana kupewa nafasi Msimbazi kuliko ilivyo kwa kiungo huyo kutoka Guinea.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *