Baada ya mechi mbili za jana Jumapili, Ligi Kuu Bara imesimama hadi Novemba 21, 2025 kupisha kalenda ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Kimataifa (FIFA) ambapo timu za taifa zitakuwa dimbani.

Kabla ya mechi mbili za jana, tumshuhudia zikipigwa mechi 37 na kupatikana jumla ya mabao mabao 66, yakiwemo yale matatu waliyozawadiwa Pamba Jiji kutokana na wapinzani wao Dodoma Jiji kushindwa kufanya mechi kuchezwa na kuvunjika.

Mechi hiyo ya Dodoma Jiji dhidi ya Pamba Jiji ilifanyika Oktoba 25, 2025, lakini haikumaliza dakika tisini, ilivunjika baada ya taa za Uwanja wa Jamhuri uliopo Dodoma kuzima na kukosekana mbadala wa kuwashwa, hivyo wenyeji wakapoteza mechi kikanuni. Wakati mechi ikivunjika, Dodoma Jiji ilikuwa ikiongoza bao 1-0.

Ligi imesimama ikiwa tayari zimechezwa raundi sita, lakini kwa baadhi ya timu, zimeshuka dimbani chini ya mechi tano ambazo ni Simba (3), Singida Black Stars (3), Azam (3), TRA United (3), Yanga (4) na Tanzania Prisons (4). Zilizobaki, zina mechi tano na sita.

Hata hivyo, katika mechi 37 kabla ya mbili za jana, imeshuhudiwa baadhi ya timu zikiwa hazina makali katika kujilinda, wala kushambulia. Zingine zipo vizuri katika kushambulia, lakini kujilinda tatizo. Kwa kifupi, matatizo ya kujilinda na kushambulia yameonekana wazi ikiwa bado ligi haijachanganya.

Msimu uliopita kipindi kama hiki baada ya kuchezwa mechi 37, yalikuwa yamefungwa mabao 65, pungufu ya bao moja kulinganisha na msimu huu kwa idadi ya mechi hizo.

Unaweza kusema ndiyo timu yenye matatizo makubwa katika Ligi Kuu Bara msimu huu. Kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Marcio Maximo, kimefunga bao moja katika mechi tano. Bao hilo lilifungwa na Rashid Chambo katika mechi ya kwanza msimu huu dhidi ya Dodoma Jiji ambayo KMC iliibuka na ushindi wa 1-0.

Chambo anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kutikisa nyavu za Ligi Kuu Bara msimu huu, lakini bao hilo, limekuwa kama na gundu kwao kwani tangu hapo, imeshuka dimbani mara nne na kutoka bila ya bao.

Ikiwa na bao moja ikiwa ni wastani wa 0.17, KMC imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita, wastani wa kuruhusu 1.2, huku ikiburuza mkia kunako msimamo wa Ligi Kuu Bara ikikusanya pointi tatu.

MTIBWA SUGAR

Imerejea Ligi Kuu Bara baada ya kushuka msimu wa 2023-2024. Hata hivyo, haijaanza vizuri kwani katika mechi tano ilizocheza, imekusanya pointi tano, ikiwa na wastani wa kukusanya pointi moja kila mechi.

Katika ufungaji, ina mabao mawili pekee, wastani wa kufunga ni 0.4, sawa na kucheka na nyavu kila baada ya dakika 225. Pia imeruhusu mabao matatu kwa wastani wa 0.6.

FOUNTAIN, COASTAL, NAMUNGO

Mabao matatu yamefungwa na timu hizo, huku Namungo ikishuka dimbani mara tano kabla ya jana kupambana na Azam. Fountain Gate ina mechi sita, huku Coastal Union inazo tano.

Namungo katika mechi tano, wastani wake wa kufunga bao kila mechi ni 0.6, huku ikiwa imeruhusu mabao sita kwa wastani wa 1.2. Ina pointi tano kwa wastani wa pointi moja kila mechi. Ina wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 150.

Fountain Gate iliyoanza mechi tatu ikiwa na wachezaji pungufu, kwa sasa kama imejipata kwani haijapoteza tatu zilizofuata ikishinda mbili na sare moja.

Katika mechi sita ilizocheza, imefunga mabao matatu kwa wastani wa 0.5, imeruhusu saba kwa wastani wa 1.17. Pointi ilizokusanya saba. Ina wastani wa kufunga bao kila baada ya dakika 180.

Coastal Union katika kufunga kama Namungo, lakini katika kuzuia, imeruhusu mabao matano kwa wastani wa bao moja kila mechi.

DODOMA JIJI, MASHUJAA

Zote zikiwa zimeshuka dimbani mara sita, zimefunga mabao manne kila moja kwa wastani wa 0.7 ambapo ni kila baada ya dakika 135 wanacheka na nyavu.

Mashujaa katika mechi sita, imekusanya pointi nane, ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne. Kwa kifupi, ina uwezo mzuri wa kushambulia, lakini haina uwezo wa kuzuia kwani idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa ni sawa.

Dodoma Jiji yenye pointi tano katika mechi sita, imeruhusu mabao saba, wastani wa nyavu zao kutikiswa ni 1.17 kwa mechi.

PAMBA JIJI, MBEYA CITY

Mabao ya kufunga na kufungwa kwa timu hizi yanafanana, kila moja imefunga saba na kuruhusu sita. Pamba Jiji ikikusanya pointi tisa, wakati Mbeya City inazo nane katika mechi sita kila moja.

Zina wastani wa kuruhusu bao moja kila mechi, huku upande wa kufunga wastani ukiwa ni 1.17, ambapo kila baada ya dakika 77 zina uwezo wa kutikisa nyavu.

 JKT TANZANIA

Balaa lipo hapa, Wanajeshi hawa wamefunga mabao manane na kuruhusu idadi hiyo. Ina makali katika kucheka na nyavu ikiwa ndiyo timu yenye mabao mengi sawa na Simba, lakini katika kujilinda, pia inaongoza kwa nyavu zake kutikiswa zaidi, hii ni kabla ya mechi za jana Jumapili.

Kwa wastani, JKT Tanzania ina uwezo wa kufunga kila baada ya dakika 68, kila mechi wastani wa kufunga ni 1.3.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *