Taarifa ya shirika hilo la kimataifa la msalaba mwekundu imekumbushia kwamba kwa miaka sasa jimbo la Ituri limeendelea kuwa mizozo inayojirudia kutokana na mashambulizi ya makundi yenye silaha, operesheni za mara kwa mara za kijeshi kukabiliana na makundi hayo huku haya yote yakisababisha usalama mdogo kwa wananchi ambao sasa wanaendelea kuwa katika tishio lisilo na kikomo.
Shirika hilo la kimataifa pia lina wasiwasi kuhusu upungufu wa upatikanaji wa huduma za afya na kuongezeka kwa idadi ya majeruhi wa kila mara kutokana na ghasia za mara kwa mara katika jimbo hilo. Mfanyakazi wa shirika hilo la msalaba mwekundu katika jimbo ni Ituri Alfred Wadie anasema kuwa wananchi ndiyo wanaoteseka zaidi kutokana na migogoro hii.
“Mzunguko huu umedhuru sana uwezo wa watu kujitegemea kwa njia za kujikimu katika makazi yao, umedhoofisa sekta ya kilimo, suala ambalo linaufanya ukosefu wa chakula kuwa mgumu zaidi, lakini kubwa zaidi unaathiri pia sekta ya huduma za afya kwa kukosa nguvu kazi kwa sababu watalaam wa afya wote wametoroka. Pia kuna ukosefu wa vifaa vya afya na madawa.”
Hali katika jimbo hilo la Ituri imeendelea kuwa ya woga kutokana na uwepo mwingi wa makundi yenye silaha miongoni mwao yakiwa ni makundi ya CODEMO, ADF la nchini Uganda, CRP na jingine linalojulikana kama Zaire. Makundi haya yameifanya hali ya usalama kudorora na wananchi kuendelea kuwa katika hatari nyumba zao zikiendelea kuteketezwa kwa moto, mauaji ya mara kwa mara na mfumo mzima wa huduma za kijamii kutatizika kwa ujumla.
Dieudonné Lossadhekana mkuu wa shirika la kiraia jimboni Ituri maarufu vives de l’Ituri, anasema ni kama hata jumuiya ya kimataifa umeusahau mzozo wa Ituri. “Kulingana na uharibifu, mauaji na uhalifu mkubwa unaoendelea jimboni Ituri,wasiwasi wetu ni kwamba hata jamii ya kimataifa ambayo inawakilishwa vizuri tu jimboni Ituri na ujumbe wa amani wa MONUSCO hauna tatizo hili. Tunataka ulimwengu angalau utambue kuwa maisha yanaendelea kuathirika Ituri bila hukumu yoyote kwa wahusika.”
Mzozo wa matumizi ya silaha katika jimbo la Ituri pia umeendelea kuacha makovu na kuathirika kisaikolojia kwa wakazi wa jimbo hilo, huku mauaji, kuachana kwa familia na hofu kubwa ya usalama vimeendelea kuwa donda ndugu kwa raia na kuishia kuwa na msongo wa mawazo usioisha.
Mnamo mwezi Mei mwaka 2021, hali ya dharura ilitangazwa huko Ituri chini ya amri ya rais Félix Tshisekedi ili kukabiliana na hali ya usalama mdogoisiyoisha kutokana na uwepo mwingi wa makundi ya silaha mashariki Congo. Miaka minne baadaye, ghasia za mauaji na silaha zinaendelea hasa katika eneo la Djugu, ambapo mashambulio zaidi ya mia moja yameripotiwa mwaka 2024.
