Nchini Tanzania, viongozi waandamizi wa chama cha upinzani CHADEMA wameachiwa huru kwa dhamana, baada ya kukamatwa na polisi siku kadhaa zilizopita, wakihusishwa na machafauko yaliyokumba nchi hiyo wakati wa uchaguzi mkuu Oktoba tarehe 29 mwezi uliopita.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Walioachiwa ni pamoja na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho kwa upande wa Tanzania Bara John Heche, ambaye alikamatwa siku chache kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi Oktoba na kufunguliwa mashtaka ya ugaidi.
Wengine ni Naibu Katibu Mkuu wa chama hichoTanzania Bara Amani Golugwa, Mwenyekiti Kanda ya Pwani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama Boniface Jacob na Mjumbe wa Kamati Kuu Godbless Lema.
Licha ya kuachiwa huru, viongozi hao wanatarajiwa kuripoti katika kituo kikuu cha polisi jijini Dar es Salaam, hivi leo kwa mujibu wa wakili wa chama hicho Hekima Mwasipu.

Aidha, siku ya Jumatatu, Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, iliahirisha kusikiliza kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama hicho Tundu Lissu hadi tarehe 12 mwezi huu kwa kile kilichotajwa kuwa sababu za kiusalama.
Haya yanajiri wakati huu, rais Samia Suluhu Hassan, akiendelea kupata shinikizo za kuwaachia huru, wafungwa wote wa kisiasa na kuongoza maridhiano baada ya nchi hiyo kukumbwa na machafuko ya uchaguzi mkuu.