“Bajeti za kibinadamu zimefikia kiwango cha ukomo, na msaada wa majira ya baridi tutakaoweza kutoa mwaka huu utakuwa mdogo sana,” amesema Dominique Hyde, Mkurugenzi wa Mahusiano ya Nje wa UNHCR, ambaye amerejea hivi karibuni kutoka Syria na Jordan.

Ameongeza kuwa “Familia zitabaki zikikabiliana na baridi kali bila vitu ambavyo wengi wetu tunavichukulia kuwa vya kawaida  kama paa imara kwenye nyumba, vifaa vya kuhifadhi joto, mfumo wa kupasha nyumba joto, mablanketi, nguo za joto au dawa.”

Familia zilizoathiriwa na vita nchini Ukraine zinapokea usaidizi wa majira ya baridi kutoka kwa UNHCR na washirika.

© UNHCR/Alina Kovalenko

Familia zilizoathiriwa na vita nchini Ukraine zinapokea usaidizi wa majira ya baridi kutoka kwa UNHCR na washirika.

Ukusanyaji wa fedha kwa ajili ya msimu wa baridi

UNHCR leo imezindua kampeni yake ya kimataifa ya ukusanyaji wa fedha kwa majira ya msimu wa baridi, kusaidia familia zilizolazimika kukimbia na waliorejea katika maeneo yaliyoathirika zaidi kutimiza mahitaji yao ya dharura katika miezi ijayo.

Kampeni hii ni moja ya nyakati muhimu zaidi kwa shirika hilo katika suala la ukusanyaji wa fedha.

Mwaka huu, wakati serikali nyingi zikikata misaada kwa washirika kama UNHCR, shirika hilo limesema ni muhimu zaidi kuliko hapo awali kwa watu binafsi na wafadhili wa sekta binafsi kuchukua hatua ili kuokoa maisha wakati viwango vya baridi vikizidi kushuka.

UNHCR inapanga kukusanya angalau dola milioni 35 kusaidia kukarabati nyumba zilizoharibiwa kwa mabomu, kuweka vifaa vya kuhifadhi joto, kutoa blanketi na msaada wa joto kwa watoto na wazee, pamoja na fedha za dawa na chakula cha moto.

Hali tete Mashariki ya Kati

Katika eneo la Mashariki ya Kati, UNHCR inasema  hali bado ni tete sana, ingawa zaidi ya Wasyiria milioni moja wameweza kurejea nchini mwao tangu kuanguka kwa utawala wa Assad.

Shirika hilo linasema wengi wanarejea kwenye nyumba zilizoharibiwa vibaya kutokana na vita vya muda mrefu.

Familia zilizo hatarini zaidi zinakabiliwa na baridi kali bila ulinzi wowote, huku upungufu wa ufadhili ukihatarisha kuacha watu 750,000 bila msaada muhimu katika msimu huu  ikiwemo mablanketi, magodoro, vifaa vya jikoni, taa za sola na nguo za majira ya baridi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *