
Mkurugenzi wa tume ya haki za binadamu ya umoja wa Mataifa, Volker Türk, ametaka kufanyika uchunguzi wa kina wa mauaji na vitendo vingine vilivyotekelezwa wakati wa uchaguzi wa Octoba 29 nchini Tanzania, wito anaoutoa wakati huu ripoti zikiibuka kuwa huenda vikosi vya usalama vinachukua miili ya watu waliouawa na kuipeleka kusikojulikana.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa na tume hiyo kutoka vyanzo mbalimbali nchini Tanzania, zinaashiria kuwa mamia ya waandamanaji na raia wengine waliuawa huku idadi ya waliojeruhiwa au kukamatwa ikiwa haijulikani.
Aidha tume hiyo imesema haijaweza kuthibitisha moja kwa moja kuhusu idadi kamili ya watu waliouawa kutokana na sababu za kiusalama na kuzimwa kwa mtandao kufuatia zoezi la upigaji kura.
Ripoti za familia kuhangaika kutafuta wapendwa wao, kuzunguka kituo kimoja baada ya kingine cha polisi, hospitali moja hadi nyingine zinaogopesha. Natoa wito kwa mamlaka za Tanzania kutoa taarifa kuhusu hatma na mahali waliko watu ambao hawajulikani, kukabidhi miili ya waliouawa kwa familia zao ili wapewe heshima za mazishi,” alisema Türk.
Kuna taarifa pia za kuogofya kwamba vikosi vya usalama vimekuwa vikiondoa miili iliyokufa katika mitaa na hospitali na kisha kuipeleka katika maeneo yasiyojulikana, lengo likionekana na kuficha ushaidi.”
Mkuu wa tume hiyo ametoa wito kwa mamlaka za Tanzania kuchunguza kwa ukamilifu na uwazi matukio haya ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu, na kuwachukulia hatua waliohusika.
Kwa mara nyingine ametoa wito wa kuachiwa bila ya masharti kwa viongozi wa upinzani na wafuasi wao waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu, akiwemo mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, Pamoja na wengine wote waliokamatwa kinyume cha sheria wakati wa uchaguzi.
Kwa mujibu wa tume hiyo, wanazo tarifa kuwa watu zaidi ya 150 walikamatwa huku msingi wa kukamatwa kwao ukiwa haujulikani, wengi wao Watoto wanaodaiwa kushtakiwa kwa makosa ya uhaini.
“Ni muhimu kwa wale wote waliokamatwa au kuzuiliwa kwa tuhuma za uhalifu wapelekwe haraka mahakamani, na wapewe haki ya kupinga kushikiliwa kwao kinyume cha sheria. Wote waliokamatwa lazima wapewe haki za msingi za kisheria zilizo chini ya sheria za kimataifa,” amesema Türk.