Botswana. Unalikumbuka kundi la Makhirikhiri Traditional Group kutoka Botswana? La hasha! Utakuwa unalikumbuka kwa jinsi lilivyojizolea umaarufu mkubwa katika mataifa mbalimbali na kutoa burudani isiyosahaulika kwa nchi za Afrika, hususan Afrika Mashariki.

Kundi hilo ambalo limeundwa na Moses Malapela almaarufu ‘Shumba Ratshega’ liliwaunganisha wasanii sita; wanaume wanne na wanawake wawili.

Wimbo wao maarafu wa Makhirikhiri ambao uliwatambulisha kwa jamii, uliandikwa kwa lengo la kufikisha ujumbe kuhusiana na udanganyifu wa kimapenzi, unaosababisha kuvunjika kwa ndoa nyingi na kuenea kwa maambukizi ya Ukimwi. 

Baada ya wimbo huo kusikika kwenye vituo vya redio na televisheni. Mwaka 2010 kundi hilo likaamua kutoka Botswana ili kusafiri kwa ajili ya kuendelea kupambania muziki wao. Walifanya ziara katika nchi mbalimbali Afrika Mashariki, ikiwamo Tanzania na Malawi na kila walikopita walipokelewa kwa shangwe kubwa. 

Maonesho yao yaliwavutia watu kutokana na uchezaji wao huku nchini Tanzania wakipiga show kwenye mikoa mbalimbali ikiwamo Mwanza, Shinyanga, Dar es Salaam huku likihitimisha ziara yake mkoani Mbeya tukio ambalo lilifanyika Juni 12, 2010.

Lakini safari yao haikukosa changamoto. Kwa mujibu wa kiongozi wa kundi Shumba, aliwahi kueleza kuwa baada ya kufanya ziara na kujizolea umaarufu baadhi ya vyombo vya habari vya ndani ikiwamo Radio Botswana viliacha kupiga nyimbo zao. Jambo ambalo lilipelekea kuanza kushuka kwani kwa wakati huo redio hiyo ilikuwa ikisikika masafa marefu ndani na nje ya nchi.

Baada ya muda kundi hilo likaanza kupotea machoni mwa mashabiki. Mwaka 2017, kiongozi wao Shumba Ratshega alitangaza rasmi kuacha kuimba muziki wa asili na kuingia kwenye huduma za kiroho ambapo alijulikana kama Mchungaji Moses Malapela. 

Hata hivyo, mapenzi yake kwenye muziki hayakukoma, mwaka 2023 Shumba alirudi tena kuimba huku akibadilisha mwelekeo ambapo wakati huo alitoa nyimbo za Injili ikiwamo ‘Kamoso Ke Metholo’ na ‘Mene Mene Tekele’.

Kwa sasa kundi hilo linaripotiwa kupotea kabisa huku washiriki wake wakidaiwa kuendelea na shughuli zao nyingine huku jina la Makhirikhiri likibaki kama kumbukumbu ya enzi za muziki wa jadi kutoka Botswana.

Kundi la Makhirikhiri chini ya uongozi wa Shumba Ratshega (Moses Malapela) lilijipatia mafanikio makubwa kupitia mauzo ya nyimbo, maonesho ya kimataifa na tuzo za ndani ya nchi ikiwamo ile ya ‘Best Male Artist’. Huku ikifanikiwa zaidi katika ziara zake ambapo kila nchi walipokwenda walifanikiwa kuuza tiketi zote ‘Sold Out’.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *