Serikali za Afrika ikiwemo Tanzania, hospitali binafsi na wataalamu wa teknolojia wamehimizwa kushirikiana kuunda mikakati ya kitaifa ya huduma za afya inayotumia akili Unde.

Mikakati hiyo inapaswa kulenga kuboresha ushirikiano wa mifumo ya ukusanyaji na matumizi ya taarifa pamoja na kuwajengea uwezo watumishi wa afya katika ujuzi wa kidijitali.

Kwa sasa, hospitali na taasisi nyingi za afya barani Afrika zimeanza kutumia teknolojia za akili Unde kusaidia kupanga vipaumbele vya wagonjwa, kutabiri milipuko ya magonjwa na kurahisisha utambuzi wa maradhi kwa haraka. 

Wataalamu wanasema endapo mwelekeo huu utaendelezwa, Afrika inaweza kuwa mfano wa dunia katika kutoa huduma za afya za kisasa, jumuishi na zenye kumweka binadamu mbele ya teknolojia.

Aidha, wamependekeza utekelezaji wa mwongozo wa bara wa kukuza uelewa wa akili Unde pamoja na kuongeza uwekezaji katika kampuni changa za teknolojia na miundombinu yake.

Wanasema hatua hiyo itasaidia bara la Afrika kuwa na uhuru wa kiteknolojia na kuchochea ubunifu endelevu.

Mwenyekiti na Mkurugenzi Mtendaji wa Mkutano wa Kilele wa Akili Unde Afrika (APAIC 2025), Abdulwahid Ali Khamis, amesema sekta ya afya barani Afrika kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na changamoto za uhaba wa fedha, wafanyakazi na miundombinu, lakini mabadiliko mapya yanaanza kuonekana na huenda yakalifanya bara hilo kuwa kinara katika ubunifu wa huduma za afya za kidijitali.

“Teknolojia ya kizazi kipya ya akili Unde inayoitwa Agentic AI imepiga hatua kubwa. Sasa siyo tu kuchambua taarifa, bali inaweza kufanya maamuzi, kuchukua hatua na kushirikiana na binadamu kwa wakati halisi. Badala ya kuchukua nafasi ya binadamu, teknolojia hii inakuwa mshirika anayesaidia madaktari, wasimamizi wa hospitali na maafisa wa afya,” amesema.

Ameongeza kuwa wingi wa vijana barani Afrika, ukuaji wa miundombinu ya kidijitali na ongezeko la wataalamu wa teknolojia ni fursa kubwa. 

Kwa sasa, wabunifu wengi wanaunda hospitali za kisasa zilizounganishwa na mifumo ya akili bandia, maabara zenye uwezo wa kidijitali na programu za afya za jamii zilizounganishwa mtandaoni.

Alitoa wito kwa serikali, sekta binafsi, wawekezaji, taasisi za elimu na wadau wa maendeleo kuungana na kushiriki mkutano wa APAIC 2025 utakaofanyika jijini Arusha, ambako kutasainiwa tamko maalum la kimataifa kuhusu matumizi salama na yenye maadili ya akili bandia katika huduma za afya.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa mafanikio ya matumizi ya teknolojia hiyo yanahitaji uwekezaji mkubwa katika miundombinu ya taarifa, viwango vya maadili, na mafunzo ya kidijitali kwa wataalamu wa afya.

 Baadhi ya hospitali tayari zimeanza kutumia mifumo hiyo, ikionesha jinsi teknolojia inavyoweza kusaidia kuboresha utendaji bila kupunguza umuhimu wa utaalamu wa kibinadamu.

“Kwa kutumia akili bandia katika kazi za kawaida, madaktari wanapata muda zaidi wa kuwahudumia wagonjwa. Katika dharura, mifumo hiyo inaweza kubadilisha taarifa kuwa hatua za haraka, jambo linaloweza kuokoa maisha,” amesema.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuzingatia maadili katika matumizi ya teknolojia hiyo, akibainisha kuwa viongozi wa teknolojia barani Afrika wanaendelea kuweka kanuni za kulinda faragha za wagonjwa, usalama wa taarifa na upatikanaji sawa wa huduma za kiteknolojia.

Mkutano wa APAIC 2025 utakaofanyika Arusha unatarajiwa kuwa jukwaa kubwa la kujadili maendeleo ya akili bandia na mageuzi ya kidijitali barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *