Dar es Salaam. Wakulima 120 kutoka wilaya mbalimbali za mkoa wa Ruvuma wamenufaika na mafunzo ya kilimo bora na chenye tija yaliyoandaliwa na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), yenye lengo la kuongeza uzalishaji na ufanisi katika sekta ya kilimo-biashara.

Mafunzo hayo, yaliyohusisha wakulima kutoka Songea Mjini, Songea Vijijini, Namtumbo na Madaba, yalifunguliwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Ahmed Ahmed, ambaye ameishukuru benki hiyo kwa mchango wake katika kuinua kilimo mkoani humo.

Mkuu wa mkoa wa Ruvuma, Brigedia Ahmed Ahmed

Brigedia Ahmed amesisitiza umuhimu wa wakulima kutumia maarifa waliyopata ili kubadilisha kilimo chao kiwe cha kisasa na chenye faida zaidi.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Faithful Joshua, Afisa Mwandamizi wa Huduma kwa Wateja wa TADB, amesema miongoni mwa mada kuu zilizojadiliwa ni pamoja na huduma na bidhaa za benki hiyo, urasimishaji wa kilimo-biashara, na elimu kuhusu Mfuko wa Dhamana ya Mikopo kwa Wakulima Wadogo (SCGS).

Ameongeza kuwa washiriki walijadili pia hali ya kilimo, ufugaji na uvuvi katika wilaya husika pamoja na uimarishaji wa vyama vya ushirika na AMCOS.

“Washiriki walikuwa wakulima kutoka vikundi mbalimbali ikiwemo Nakaheguo Group, Nalima AMCOs, Lumbingu Farmers, Juhudi Mpitimbi Farmers, Luganga Farmers, Ngoni Organized Farmers Group, na Umatengo Farmers Group,” amesema Joshua.

Kwa upande wake, Ashura Akim, Afisa Mwandamizi wa Maendeleo ya Biashara wa TADB, ametaja kuwa walihudhuria pia wakulima binafsi kutoka maeneo ya Mtyangimbole, Mbinga Muhalule, Litisha, Nakahuga, Matomondo, Msamala, Namtumbo na Mshangano, pamoja na wajasiriamali wa Ruvuma Mwalu.

Wakulima walioshiriki waliishukuru TADB kwa kuandaa mafunzo hayo, wakisema yamewapanua uelewa kuhusu huduma na fursa zinazotolewa na benki hiyo, na jinsi wanavyoweza kunufaika nazo ili kuboresha shughuli zao za kilimo-biashara.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *