Wachezaji wa Timu ya taifa ya Nigeria wamesitisha mgomo wao mfupi na kurejea mazoezini baada ya mzozo baina yao na Shirikisho la Soka la Nigeria (NFF) kuhusu stahiki zao ambazo hawajalipwa siku chache kabla ya mechi yao ya mchujo ya kuwania kufuzu Kombe la Dunia la FIFA 2026 dhidi ya Gabon jijini Rabat, Morocco.

Mgomo huo ulianzishwa juzi Jumatatu lakini baada ya majadiliano, wachezaji hao wameamua kucheza mechi hiyo dhidi ya Gabon.

Nahodha wa Nigeria, William Troost-Ekong, amethibitisha kutokea kwa tukio hilo katika ukurasa wake wa X, akiwahakikishia mashabiki kuwa umoja umerejeshwa ndani ya kikosi.

“Suala limetatuliwa. Tuko pamoja na kama hapo awali tumezingatia michezo iliyo mbele yetu! 🇳🇬 @NGSuperEagles,” mlinzi huyo ameandika.

Mabingwa hao mara tatu wa Afrika siku ya Jumatatu na Jumanne walisusia vikao vya mazoezi ili kudai bonasi za mechi ambazo hazijalipwa na posho za kambi.

Wachezaji hao waliripotiwa kusikitishwa na kile walichokitaja kama “ahadi zinazojirudfa zisizotimizwa” kutoka kwa NFF licha ya kuhakikishiwa hapo awali.

Mzozo wa stahiki zisizolipwa si jambo geni kwa timu ya taifa ya Nigeria katika miaka ya hivi karibuni

Mara kwa mara wachezaji wa timu hiyo wamekuwa wakiingia katika mizozo na NFF kuhusu madai yao.

Wakati wa Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2021 nchini Cameroon, inasemekana wachezaji walisubiri kwa miezi kadhaa kabla ya kupokea posho za kambi na bonasi.

Ucheleweshaji kama huo wa malipo ulirekodiwa baada ya mechi za kufuzu AFCON 2023 na kampeni ya kufuzu AFCON 2025, huku posho za mechi za kirafiki bado hazijalipwa.

Mnamo Machi 2024, wachezaji wakuu walionyesha wasiwasi wao kwa kificho juu ya kile walichokiita “utamaduni wa kupuuza” kuhusu ustawi, hata kama timu iliendelea kufikia malengo ya ushindani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *