Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa unashirikiana kwa karibu na Halmashauri Kuu ya Umoja wa Afrika katika kuoanisha ajenda zao kuu za maendeleo — Ajenda 2063 ya Afrika na Ajenda 2030 ya Umoja wa Mataifa — kwa lengo la kumaliza migogoro barani Afrika na kuhakikisha uwakilishi wa haki zaidi katika taasisi za kimataifa, hususan Umoja wa Mataifa.

Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Mahmoud Ali Youssouf, amesema taasisi hizo mbili zinaendeleza ushirikiano wa karibu katika programu muhimu za amani, hasa kupitia mpango wa bara la Afrika wa “Kukomesha Milio ya Bunduki Barani Afrika kufikia mwaka 2030.”

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema ushirikiano huo wa kimkakati umewezesha kuundwa kwa mfumo wa pamoja wa amani na usalama, ambao umeimarisha juhudi za pamoja kuanzia hatua za awali za kuzuia migogoro hadi katika mchakato wa kujenga amani baada ya migogoro.

Guterres ameongeza kuwa makubaliano hayo yanatoa msukumo kwa bara la Afrika kupewa viti vya kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, akilitaja hilo kuwa ni hatua ya kurekebisha kile alichokiita “dhulma isiyovumilika ambayo bara la Afrika limekuwa likikumbana nayo kwa muda mrefu.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *