Ripoti inasema uzalishaji wa ngano na nafaka mbichi duniani unaelekea kuweka rekodi mpya, vivyo hivyo na uzalishaji wa mchele barani Asia na katika kanda ya Amerika ya Kusini na Karibea.

Uwiano wa akiba na matumizi kwa mazao haya muhimu pia unatarajiwa kuongezeka, kulingana na ripoti hiyo mpya ya FAO .

Ripoti hiyo ya kila nusu mwaka hutoa tathmini na utabiri wa soko kuhusu uzalishaji, matumizi, biashara na akiba ya bidhaa kuu za chakula ikiwemo nafaka, mazao ya mafuta, sukari, nyama, maziwa, na samaki.

Toleo hilo jipya pia linatoa uchambuzi wa ziada kuhusu soko la mafuta ya mizeituni, masoko ya mbolea, na gharama ya uagizaji wa chakula duniani.

Kuimarika kwa uzalishaji wa chakula duniani ni hatua chanya kwa uthabiti wa masoko. Hata hivyo, nyuma ya takwimu hizi bado kuna hatari zinazoendelea  kuanzia mabadiliko ya tabianchi hadi uhusiano dhaifu wa kibiashara ambazo zinaweza kubadilisha kwa haraka upatikanaji na usambazaji wa chakula duniani. Kujenga mnepo katika mfumo mzima wa chakula na kilimo ndiyo changamoto yetu kubwa zaidi,” amesema Mchumi Mkuu wa FAO, Maximo Torero.

Ripoti imeongeza kuwa masoko ya ngano, mahindi, na mchele yanaonesha uwepo wa akiba kubwa inayoweza kuuzwa nje, hali ambayo imesababisha kushuka kwa bei katika masoko ya kimataifa.

Wakati huo huo, imesema matumizi ya ngano na hasa mchele yanatarajiwa kuongezeka kwa kiasi kikubwa, yakichochewa na ongezeko la matumizi katika nchi zenye kipato cha chini na upungufu wa chakula (LIFDCs).

Nyama ikiwa katika soko la Hamarwayne, Mogadishu Somalia. (Maktaba)

AMISOM/Omar Abdisalan

Nyama ikiwa katika soko la Hamarwayne, Mogadishu Somalia. (Maktaba)

Mambo muhimu kutoka katika uchambuzi wa bidhaa mbalimbali:

Kwa mujibu wa ripoti hiyo

·        Akiba ya ngano duniani inatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 3.6 katika mwaka ujao, kufikia kiwango cha juu zaidi kufikia mwishoni mwa msimu wa 2026, huku akiba ya mchele duniani ikitabiriwa kuongezeka kwa asilimia 2.2, ikifikia rekodi mpya.

·        Uzalishaji wa nyama duniani unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 1.4, unaoongozwa na kuku, ilhali uzalishaji wa nyama ya ng’ombe unaweza kupungua kutokana na kupungua kwa mifugo nchini Brazili na Marekani.

·        Akiba ya sukari duniani inatarajiwa kuongezeka kutokana na mavuno makubwa nchini Brazili, pamoja na matokeo mazuri ya India na Thailand, ambayo yataongeza uzalishaji kwa kasi kuliko matumizi.

·        Matumizi ya mafuta ya mimea duniani, kwa upande mwingine, yanatarajiwa kuzidi uzalishaji, hasa kutokana na kupungua kwa mazao ya soya nchini Argentina, India, Ukraine na Marekani, ambako maeneo ya kilimo yamepungua.

·        Uzalishaji wa samaki na ufugaji wa majini duniani unatarajiwa kuongezeka kwa asilimia 1.7, huku matumizi ya vyakula kutoka kwenye ufugaji wa majini yakiongezeka kwa asilimia 2.5 kwa kila mtu, kufidia kupungua kwa matumizi kutoka kwenye uvuvi wa baharini.

Taswira kuhusu mwenendo wa mafuta ya zeituni na soko la mbolea

Ripoti hiyo ya mtazamo wa chakula duniani inabainisha kuwa soko la mafuta ya mizeituni  linatarajiwa kuimarika baada ya ukame uliopunguza mavuno na kuongeza bei.

FAO inasema bei zimepungua kwa zaidi ya nusu nchini Hispania na Ugiriki, huku Italia bado ikiwa juu. Tunisia inaweza kuwa mtayarishaji wa pili kwa ukubwa duniani msimu wa 2025/26 kutokana na mvua nyingi na mavuno ya rekodi.

Bei za chini zinachochea matumizi, na biashara ya kimataifa inaweza kufikia kiwango cha juu kihistoria, ingawa ushuru wa Marekani unaweza kupunguza kiasi cha jumla imesema ripoti

Kwa upande wa mbolea, ripoti imebainisha kuwa matumizi duniani yameongezeka msimu wa 2024/25 baada ya upungufu wa awali.

Bei ya wastani ya kikapu cha mbolea ilikuwa dola 489 kwa tani Septemba 2025 ikiwa ni pungufu ya 40% kutoka Aprili 2022, lakini bado iko juu kuliko 2024.

Upatikanaji wa mbolea za nitrojeni unatarajiwa kubaki wa kutosha, ukiungwa mkono na kurejea kwa China kwenye masoko ya dunia kwa mauzo ya nje ya 2025 na 2026.

Gharama ya uagizaji wa chakula duniani

Ripoti hiyo inakadiria kuwa gharama ya uagizaji wa chakula duniani (FIB) mwaka 2025 itapanda karibu asilimia 8, kufikia dola trilioni 2.22, kutokana na ongezeko la bei za bidhaa za thamani kubwa kama kahawa na kakao, hasa kwa nchi zenye kipato cha juu.

Nchi maskini zaidi zinatarajiwa kuona ongezeko la asilimia 58 katika matumizi ya mafuta ya wanyama na mimea, kutokana na bei za juu za mafuta ya mchikichi, jambo linalozua wasiwasi kuhusu uwezo wa kumudu bei.

Kwa upande mwingine, bei za nafaka na sukari zinazoanguka zitapunguza jumla ya gharama za uagizaji wa bidhaa hizo.

Jumla, nchi zenye kipato cha chini zitaona kupungua kidogo kwa FIB, huku  Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara  ikitarajiwa kuongezeka kidogo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *