Mshambuliaji wa zamani wa Man United, Eric Cantona amemponda mmiliki mwenza wa klabu hiyo ya England, Sir Jim Ratcliffe akidai anaharibu alama iliyoachwa na meneja wa zamani wa timu hiyo, Sir Alex Ferguson.
Maoni hayo ni muendelezo wa ukosoaji ambao Cantona ameendelea kuufanya kwa uongozi wa Man United chini ya Ratcliffe.
Cantona amesema kuwa kinachofanywa na uongozi wa Ratcliffe ni kuharibu sifa zote nzuri ambazo Sir Alex Ferguson alikuwa nazo ndani ya klabu hiyo.
“Sir Alex Ferguson alitengeneza staili nzuri ya soka la kushambulia. Ambayo Mmiliki mpya angeendelea kuitumia lakini ameiharibu,” amesema Cantona.
Cantona amesema kuwa Ratcliffe anaonekana hapendi kushauriwa na amekuwa akifanya maamuzi ambayo yanaigharimu timu.
Amedai kuwa yeye mwenyewe Cantona, aliwahi kumshauri mipango mizuri ya kuifanya timu hiyo kuwa na makali yake ya zamani lakini bosi huyo hakuifanyia kazi.
“Nina hisia na mipango mingi lakini nahisi miaka miwili au mitatu iliyopita niliiweka pembeni na kujaribu kuipa kitu hii klabu ambayo imenipa kila kitu.
“Lakini (Ratcliffe) hakuonyesha kuvutiwa nayo. Nilifanya kile ambacho nilitakiwa kufanya na sijihisi mwenye hatia kwa vile nilijitahidi kadri ya uwezo wangu,” amesema Cantona.
Kabla ya kumtuhumu kuharibu alama zilizoachwa na Ferguson, Cantona aliwahi kumshambulia Ratcliffe kwa mpango wake wa kujenga Uwanja mpya wa Manchester United akidai utapoteza historia ya klabu hiyo.
Cantona aliwahi kuchezea Man United kuanzia mwaka 1992 hadi 1997 na kuifungia mabao 82 katika michezo 185.