
Dar es Salaam. Wakati msimu wa nne wa Mbio ya Rombo Marathon ukitarajiwa kushirikisha wakimbiaji 2500, tofauti na misimu iliyopita, msimu huu mbio hiyo itafanyika kwa siku tatu mfululizo.
Tamasha la mbio hiyo litaanza Desemba 22, 2025 kwa washiriki kufanya utalii chini ya mlima Kilimanjaro, katika misitu ya Kinapa kupitia muongozo wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).
Katibu mkuu na mratibu wa mbio hiyo, Similwa Mdumbwa amesema Desemba 23 itakuwa ndiyo siku ya mbio, ambayo washiriki watachuana katika umbali wa kilomita 5, 10 na kilomita 21 (nusu marathoni).
Mbio itaanzia na kumalizikia kwenye viwanja vya Kilombelo, Rongai Forest, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro ikishirikisha wakimbiaji zaidi ya 2500.
Akizungumza katika uzinduzi wa mbio hiyo uliofanyika Novemba 13, 2025 jijini Dar es Salaam, Mdumbwa amesema Rombo Marathon yenye kauli mbiu ya “Mbio na Burudani” itakwenda sanjari na tukio la
Ndafu Festival.
“Itakuwa ni zaidi ya mbio, watu warapata fursa ya kula vyakula vya asili na kinywaji aina ya mbege mara baada ya mbio ndio sababu kauli mbiu yetu ni mbio na burudani,” amesema.
Amesema Desemba 24, itakuwa ni hitimisho la Rombo Marathon ambayo wakimbiaji wote watashiriki kupanda miche ya miti 10,000kwenye eneo la chini ya Mlima Kilimanjaro.
“Rombo Marathon na Ndafu Festival ni zaidi ya mbio, linakwenda kuwa jukwaa la kuimarisha umoja, kudumisha utamaduni wa eneo letu, kukuza vipaji na kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania,” amesema Mdumbwa.
Amesema usajili wa washiriki unaendelea kwenye tovuti yao na kwenye baadhi ya vituo vya Dar es Salaam na nje ya Dar es Salaam ambako kuna matawi ya benki wadhamini wa mbio hiyo ikiwamo mdhamini mkuu, KCB na benki ya Mwanga Hakika.
“Gharama ya ushiriki ni Sh40,000 kwa kila mshiriki kwa umbali wowote,” amesema.
Akifafanua sababu za kufanyika siku tatu mfululizo, Mdumbwa amesema msimu huu ni mara ya kwanza kufanyika kwa siku tatu, akibainisha kwamba waandaaji wamependekeza hivyo kutokana na maoni ya washiriki katika misimu iliyopita.
“Siku moja ya mbio na kufanya utalii haikutosha, hivyo washiriki wakaomba tuongeze siku na kama tulivyosema Rombo Marathon ni zaidi ya mbio, inazidi kujiimarisha katika sekta ya michezo, utamaduni, utalii na uchumi na kuwaleta watu pamoja,” amesema huku akiitaja benki ya KCB kama wadhamini wakuu.
Mwakilishi wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Felix Chunga amesema mbio ya Rombo Marathon imekuwa chachu ya kuibua na kuendeleza vipaji vya riadha nchini.
“Imeendelea kufanya vizuri, ikitoa zawadi kwa washindi na kuwavutia wanariadha wengi kushiriki, kupima muda wao na washindi kuondoka na zawadi mbalimbali kutoka kwa waandaaji.
“Imekuwa moja ya mbio yenye mchango mkubwa katika ustawi wa wanariadha wetu, kama haitoshi imekuwa ikileta watalii, jambo linalozidi kuifanya kuwa kubwa,” amesema.