
Washirika wa biashara barani Afrika wamethibitisha kujitolea kwao kuendeleza ushirikiano kati ya watunga sera, wawekezaji, wavumbuzi na viongozi wa sekta ya fedha, kwa kutilia mkazo mkubwa maendeleo ya ujumuishaji wa kifedha kupitia teknolojia.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika mkutano uliofanyika hivi karibuni jijini Nairobi, Kenya, wadau walikubaliana kuwa juhudi hizo zitaelekezwa katika kuimarisha elimu ya fedha, kuendeleza biashara ndogo na za kati (MSMEs), pamoja na kukuza bunifu za kifedha zinazolenga kuwawezesha wananchi, hususan wanaoishi katika maeneo ya vijijini.
Ean Luc Nzoubou, Mkurugenzi Mkuu wa Advance Congo, anasema maendeleo barani Afrika yanaendelea kuimarika mwaka baada ya mwaka, huku kukiwa na fursa nyingi na matumaini makubwa ya siku zijazo. Licha ya hatua nzuri zilizopigwa ikilinganishwa na miaka 10–20 iliyopita, bado kuna mambo yanayohitaji kufanyiwa kazi ili kuimarisha uchumi zaidi.
‘‘Mikutano kama hii ni muhimu kwa kufanya tathmini ya tulipotoka, kupanga mkakati wa siku zijazo na kubaini njia bora za kuboresha shughuli na huduma za kifedha katika nchi mbalimbali za Afrika.’’ Alisema Ean Luc Nzoubou, Mkurugenzi Mkuu wa Advance Congo.
Naye Guillaume Valence, Mkurugenzi Mkuu wa Advance Ghana, anasisitiza kuwa teknolojia inapaswa kutumika kuboresha huduma za kifedha bila kuchukua nafasi ya binadamu, hasa katika elimu ya fedha. Anabainisha umuhimu wa kuwapa wananchi ujuzi wa usimamizi wa fedha na kuhakikisha huduma hizo zinawafikia popote walipo.
‘‘Mfumo wa “high-tech, high-touch” ndio njia bora ya kuchanganya teknolojia na uhusiano wa kibinadamu ili kujenga mifumo imara ya kifedha na, mataifa yanapaswa kuwekeza katika miundombinu kama mtandao na barabara ili kuwawezesha wananchi kustawi kiuchumi’’Alisema Valence
Kwa mujibu wa wadau, mustakabali wa Afrika katika ujumuishaji wa kifedha utategemea kwa kiasi kikubwa uwekezaji katika teknolojia, ushirikiano wa kikanda, na kuweka watu-hasa wale walioko maeneo yenye changamoto za miundombinu-katika kiini cha ubunifu wa kifedha.