Majadiliano ya hii leo Jumamosi kwenye mkutano huo yalilenga uhamasishaji wa fedha kile viongozi wamekiita “injini ya mabadiliko ya tabianchi.” Kwa mataifa mengi yanayokumbwa na athari, ufadhili si suala la chaguo, bali “suala la kuishi.”

Katika ufunguzi wa Mazungumzo ya Tatu ya Ngazi ya Juu kuhusu Ufadhili wa Tabianchi, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, ameeleza kuwa COP30 inapaswa kuwa mwanzo wa kutekeleza hadi ya dola trilioni 1.3 kwa mwaka katika ufadhili wa tabianchi, fedha ambazo zinapaswa “zifike kwa wanaozihitaji zaidi, kwa haraka, kwa uwazi na kwa usawa.”

Amesisitiza kuwa hatua za tabianchi na haki ya kijamii ni “mambo yasiyotenganishwa,” akionya kuwa mzunguko wa ukosefu wa usalama wa tabianchi, njaa, umaskini, uhamaji na migogoro unapaswa kukatwa ili kufikia malengo ya kimataifa.

Bi. Baerbock alikumbusha pia hatua zilizopigwa tangu Mkataba wa Paris ambapo nishati jadidifu iliyokuwa ikionekana “haiwezekani”sasa inaongoza duniani, huku uwekezaji katika nishati safi ukifikia dola trilioni 2 mwaka 2024.

Hata hivyo, alionya kuwa uwekezaji bado hauendi panapostahili, hususan Afrika, ambako zaidi ya watu milioni 600 hawana umeme licha ya bara hilo kuwa na uwezo mkubwa wa nishati jadidifu.

Rais huyo wa Baraza kuu amehimiza mataifa yaliyoendelea kutimiza ahadi zao za kiteknolojia na kifedha na kuendeleza mageuzi ya taasisi za fedha duniani.

Mafundi wakiweka paneli za umeme wa jua nchini Zimbabwe.

Mafundi wakiweka paneli za umeme wa jua nchini Zimbabwe.

Zinapoelekezwa fedha, matumaini huongezeka

Katibu Mtendaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi, Simon Stiell, naye alihutubia katika mkutano huo na kueleza kuwa ufadhili ndiyo “damu ya uhai” wa hatua za tabianchi, inayoweza kubadili mipango kuwa utekelezaji. 

Licha ya mabilioni ya fedha kuwekezwa duniani kote katika nishati safi, uthabiti na mabadiliko ya haki, Bw. Stiell alisema kiasi kinachosalia “hakitoshi wala hakitabiriki vya kutosha,” na hakigawanywi kwa usawa.

Alihimiza COP30 kuonesha tena kwamba ushirikiano wa tabianchi unafanya kazi, na kwamba uwekezaji unaofanywa sasa unaweza kuunda “hadithi ya ukuaji wa karne ya 21.”

Mkuu huyo wa masuala ya mabadiliko ya tabianchi amesisitiza kuwa “Fedha zinapotiririka, matamanio hukua,” kuwezesha utekelezaji ambao hutengeneza nafasi za kazi, unapunguza gharama ya maisha, unaboresha matokeo ya afya, unalinda jamii na kupata sayari thabiti na yenye mafanikio kwa wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *