Dar es Salaam. Katika maisha kuna ndoto ambazo huja mapema, lakini safari ya kuzifikia huchukua muda, na pia unahitaji uamuzi mgumu na kujitoa kwa kiwango cha juu kama ilivyokuwa kwa Lulu Diva, staa wa muziki na filamu.

Ndiyo, ni Lulu Diva ambaye leo hii anasimama kama mmoja wa wanawake waliopigana kwa hali na mali kwa lengo la kujiweka kwenye ramani ya sanaa hapa Bongo na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Kwa mujibu wa mahojiano mbalimbali aliyofanya, tunapata picha kuwa safari yake ilikuwa imejaa mitihani, uamuzi wa ujasiri, na hatua ambazo wanawake wengi katika tasnia wamekuwa wakisita kuzichukua.

Kabla ya jina lake kuanza kutajwa katika muziki, Lulu Diva alikuwa na maisha tofauti kabisa ambayo ingekuwa vigumu kutabiri kuwa leo angekuwa hapa alipo kiasi cha kumzungumzia.

Mrembo huyu alikuwa akihudumu katika sekta ya Hotel Management, taaluma ambayo ingeweza kumpatia ajira ya kudumu na tulivu huku akichukua mshahara wa kila mwisho wa mwezi.

Hata hivyo, ni wazi kuwa ndani ya moyo wake kulikuwa na kiu ya sanaa, hamu iliyokua taratibu tangu akiwa mwanafunzi wa Green Acres, akivutiwa na sauti za wasanii maarufu Bongo na hata kimataifa.

Miongoni mwao ni Lady Jaydee, Vanessa Mdee, Beyonce na Celine Dion, staa ambaye mwaka 2009, alitajwa na Los Angeles Times kama msanii aliyeingiza fedha nyingi kwa muongo huo ambazo ni Dola748 milioni.

Pindi ndoto yake ilipoiva, Lulu Diva akajirusha kwenye uwanja wa burudani akianza na uigizaji, kazi ambayo anaifanya hadi sasa akicheza tamthilia mbalimbali ikiwemo Jua Kali.

Filamu ya kwanza kucheza, Nikabu (2016), ndio ilimpa nafasi ya kuonja jukwaa la tasnia hiyo na kumfungulia milango ya kujulikana na mashabiki wengi.

Ili kufikia hatua hii muhimu, ilimbidi Lulu Diva kusaidiwa na Kitale a.k.a Mkude Simba ambaye alimpa mwanga na uelewa wa namna ya kusimama mbele ya kamera.

Shughuli zake kwenye uigizaji zilimfungulia mlango mwingine, nao ni kuwa video vixen, hatua ambayo wasanii wengi wa kike hasa kwenye Bongofleva waliipitia huko nyuma.

Mtu wa kwanza kumwamini katika eneo hilo alikuwa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, aliyempa nafasi ya kuonekana kwenye video ya mwanamuziki aliyekuwa anamsimamia katika lebo yake.

Video hiyo ni ya wimbo, Naogopa (2016) wake Mirror, msanii aliyesainiwa Endless Fame Label, yake Wema. Na hii ilikuwa nafasi ya kwanza kwa Lulu Diva kupenya kwenye macho ya hadhira kubwa maana video hiyo ilipokewa vizuri.

Licha ya mafanikio hayo, ndani ya Lulu kulikuwa na ndoto ambayo haikuwahi kupotea, nayo ni kuwa mwanamuziki, ndoto ambayo anaiishi kwa sasa akiwa na nyimbo nyingi maarufu.

Wimbo wake wa kwanza, Milele (2016), uliandikwa na Barnaba huku wakishirikiana pia, ulimtambulisha vizuri kwa kiasi chake, mradi uliokuja baada ya wawili hao kukutanishwa na Belle 9.

Safari hiyo ilianza taratibu, lakini kwa mtiririko wa kitaalamu kama kufanya mazoezi ya sauti, kurekodi, kujenga utambulisho wa kisanii, yaani chapa kupitia vyombo vya habari na mitandao.

Wimbo wake wa pili, Usimwache (2017), uliandikwa na Daxo Chali, mmoja wa watayarishaji muziki wenye jina kubwa akitokea MJ Records, na ndiye alihusika katika kuutengeneza wimbo huo.

Hadi kufikia hapa, Lulu Diva alionyesha kuwa hayuko kwenye muziki kwa bahati mbaya, kitu kilichofanya kupata menejimenti nzuri ambayo ilifanikisha hata video za nyimbo zake baadhi kufanyika nje ya nchi.

Kolabo yake na Rich Mavoko, Ona (2018) iliyotayarishwa na S2kizzy, ilimuweka juu zaidi, huku video ya wimbo huo ikiwa ya kwanza kwake kutazamwa zaidi ya mara milioni 1 katika mtandao wa YouTube.

Ilifuatia Extended Playlist (EP) yake ya kwanza, The 4 Some (2020) iliyounganisha wasanii wakubwa kutoka Afrika Mashariki – Fid Q (Tanzania), Eddy Kenzo (Uganda) na Khaligraph Jones (Kenya).

Hiki kilikuwa kipimo cha uwezo wake wa kwenda mbali zaidi ya mipaka, na hakika EP hiyo ilimpa heshima mpya kwenye muziki.

Kwa sasa Lulu Diva anasimama kama chapa ndani ya Bongofleva akiwa ameshirikiana na wakali wenzake kama Nandy, Country Wizzy, Mabantu, Lava Lava, Whozu, Chino Kidd, Khadija Kopa, Mr. Blue n.k. 

Akiwa na takribani miaka 10 ndani ya tasnia, Lulu Diva amejijenga vilivyo, kutoka msichana wa ndoto hadi kuwa msanii anayeheshimika kwenye muziki na uigizaji. Ila ukweli unabaki kuwa haikuwa rahisi, alijaribu kila njia – uigizaji, video vixen na muziki, ambapo kila hatua amechangia kumjenga hadi kuwa mwanamke jasiri, mchapakazi na anayeishi kwenye ndoto zake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *