Jamii ya Maban, eneo lililoko kaskazini mashariki mwa Sudan kusini ni wanufaika wa mradi huo na wametembelewa na majaji wawili wa Mahakama Kuu ambao wanafanya kazi kwa bidii kusikiliza na kuamua kesi zilizokuwa zimesubiri tangu mwaka 2020.
Video ya UNMISS inaonesha wakimbizi wakiwa kambini, Watoto wakicheza nje ya majengo yaliyoharibika. Majaji wanaonekana wakiendesha vikao vya mahakama. Mahakama hii tembezi inaleta matumaini mapya kwa jamii kwa kutoa usikilizaji wa haraka wa kesi na kuhakikisha haki inapatikana kwa wahanga na watuhumiwa.
“Ninafurahia sana kuwasili kwa mahakama tembezi. Hii ni hatua nzuri itakayowezesha kusikilizwa kwa kesi kubwa na ndogo. Waliokosa watapewa adhabu, na wasio na hatia wataachiwa huru.”
Ili kusaidia kurejesha uwajibikaji na haki huko Maban, mahakama inayotembea imetumwa kwa usaidizi wa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini (UNMISS), mahakama ya Sudan Kusini na Wizara ya Sheria na Masuala ya Kikatiba.
Katika moja ya kesi zinazoendelea, kijana mmoja akiwa amefungwa minyororo amefikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumbaka msichana mdogo. Mbele ya mahakama, mama wa mtoto huyo anaeleza maumivu anayopitia.
“Nimesikitishwa sana na kilichofanywa kwa binti yangu na naamini kijana huyu anastahili kifungo cha muda mrefu.”
Ndani na nje ya ukumbi wa mahakama, pilika zinaendelea, familia moja ikiandaa chakula, wataalamu wa ushauri nasaha wanatoa huduma muhimu kwa waathiriwa na familia zao ili kuwajenga kisaikolojia kabla ya kusimama kizimbani, mmoja wao anayeongeleshwa ni mama wa mshutumiwa.
Mshauri Kiden Scorvia, anasema “Tunawaandaa kihisia kabla ya kusikilizwa kwa kesi ili wawe na ujasiri na wawe tayari kushiriki kikamilifu wakiwa mahakamani.”
Viongozi wa jamii wanasema miongoni mwa sababu zinazopelekea ongezeko la vitendo vya ubakaji ni ndoa za utotoni, zinazodaiwa kuendelea katika baadhi ya maeneo. Juma Lagu, Kiongozi wa Jamii anasema
“Katika jamii hii, wasichana wanaolewa wakiwa chini ya umri wa miaka 18, wakati mwingine kwa kulazimishwa. Hili ni kosa kisheria na ndilo linalochangia kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji.”
Kwa upande wa UNMISS, kuna matumaini makubwa kwamba juhudi hizi zitabadilisha historia ya upatikanaji wa haki Maban. Katika siku tatu tu za mwanzo, idadi ya mashahidi na waathiriwa waliojitokeza imekuwa kubwa.
Kenneth Isaac, ni Afisa wa Utawala wa Sheria wa UNMISS, na anasema
“Katika siku tatu zilizopita, tumewaona wahanga na mashahidi wakija kusikiliza kesi zao. Wadau wote wanajitolea ipasavyo na tunatarajia ndani ya mwezi mmoja kesi zote za Maban zitakuwa zimesikilizwa.”
Nje ya mahakama, mawakili wa utetezi wanaendelea kuzungumza na familia za waathiriwa, huku baadhi ya watuhumiwa wakiwa chini ya ulinzi mkali. Licha ya hali ngumu za kijamii na kiuchumi, wananchi wa Maban wanaanza kuona nuru mpya ya haki ambayo kwa muda mrefu haikuwafikia.