Katika uamuzi uliotolewa juzi Ijumaa tarehe 14 Novemba 2025, Jopo la Majaji limesema kwamba kumsafirisha Kabuga ambaye ana ugonjwa mkali wa kusahau (dementia), udhaifu uliokithiri, na maradhi sugu mengi kutaweka maisha yake hatarini “kwa kiwango kikubwa na wazi.” Uamuzi huo umetolewa baada ya miaka ya ufuatiliaji wa kitabibu kutoka kwa madaktari wa Umoja wa Mataifa na jopo la wataalamu huru, ambao wote walionya kuwa safari ya ndege ya umbali mrefu inaweza kusababisha matatizo ya kiafya yanayoweza kuhatarisha maisha.

Kabuga amekuwa akishikiliwa katika Gereza la Umoja wa Mataifa mjini The Hague, Uholanzi tangu mwaka 2020, lakini mashitaka dhidi yake yalisitishwa kwa muda usiojulikana mwaka 2023 baada ya majaji kuamua kuwa hana tena uwezo wa kukabili mashtaka kuhusiana na nafasi yake katika mauaji ya kimbari dhidi ya Watutsi mwaka 1994.

Kwa kukosa nchi nyingine iliyo tayari kumpokea, Rwanda ilijulisha mahakama kuwa iko tayari kumchukua. Hata hivyo, wataalamu walionya kuwa hata kwa kutumia ndege maalum ya wagonjwa na timu kamili ya wahudumu, hali ya Kabuga inafanya safari ya masafa marefu kuwa hatari na inaweza kufupisha maisha yake.

Majaji walikubaliana na tathmini hiyo, wakibainisha kuwa uwezo wake wa kutembea sasa umedorora kiasi kwamba anategemea kiti cha magurudumu na anahitaji huduma za kitabibu za kupunguza maumivu pekee. Pia walisisitiza umuhimu wa kutembelewa na watoto wake mara kwa mara, wakisema kumlazimisha kuhamishwa kutakuwa na athari mbaya kisaikolojia na kiafya.

Ingawa wamekataa kumruhusu asafirishwe kwenda Rwanda, majaji wameziomba nchi za Ulaya, hasa zile ambazo Kabuga ameomba kuachiwa kwa muda, kuzingatia upya maombi yake kutokana na hali yake mbaya ya afya.

Mahakama pia imekataa ombi la Msajili wa Mahakama la kutaka kupeleka taarifa za kitabibu za Kabuga na mamlaka za Rwanda, ikisema hatua hiyo haina haja tena kufuatia uamuzi huo.

Uamuzi huu unamweka Kabuga katika hali isiyo na uhakika huku jitihada za kutafuta nchi itakayokubali na inayofaa kiafya kumpokea zikiendelea.

Kukamatwa kwa Kabuga

Felicien Kabuga ambaye anatuhumiwa kuongoza mauaji ya kimbari dhidi ya watutsi nchini Rwanda yalitotekelezwa mwana 1994 alikamatwa mwezi Mei mwaka 2020

Aliyekuwa Kamishina Mkuu wa Haki za Binadamu wakati huo Bi Michelle Bachelet aliseema, “kukamatwa kwa Félicien Kabuga, miaka 26 baada ya mauaji ya kimbari, kunasisitiza ufikiaji mkubwa wa uwajibikaji kwa makosa ya kimataifa. Hakuna ambaye anafanya makosa ya kimataifa anapaswa kufikiri kwamba kupita kwa muda kunaweza kusaidia kukwepa mkono wa haki na kwamba hawatawajibishwa.”

Kabuga alikuwa ameshtumiwa  mwaka 1997 na Mahakama ya Makosa ya Jinai ya Rwanda (ICTR) kwa makosa saba  ikiwa ni pamoja na mauaji ya kimbari, ushiriki katika mauaji ya kimbari, na pia uchochezi wa moja kwa moja na wa umma wa kutekeleza mauaji ya kimbari – yote haya yakiwa na uhusiano na uhalifu uliofanywa dhidi ya watutsi nchini Rwanda.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *