Uingereza. Wiki iliyopita mke wa lejendi wa FC Barcelona, Xavi Hernandez, 45, Nuria Cunillera alisherehekea kutimiza umri wa miaka 40, ambapo mumewe alitoa neno ambalo limebeba msingi wa makala haya kwa leo.
Xavi, mshindi wa Kombe la Dunia 2010 pale Afrika Kusini, kupitia ukurasa wake wa Instagram wenye wafuasi zaidi ya milioni 11.8, katika salamu zake alisema Nuria anastahili mambo yote mazuri duniani!
“Hongera sana mpenzi! Asante kwa kuwa mtu wa kipekee kwa kutufanya sote tuwe na furaha. Unastahili mambo yote mazuri duniani. Nakupenda sana mrembo!” alieleza Xavi.
Ni kweli Nuria, mkali mitindo mtandaoni, naye anahitahili kupata mambo mazuri kama ilivyokuwa kwa Xavi katika soka ambapo alipata mafanikio makubwa kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa.
Wawili hao walianza uhusiano wao mnamo 2012, mwaka mmoja baadaye, yaani Julai 13, 2013, Xavi na Nuria walifunga ndoa katika sherehe kubwa na ya kifahari huko Girona, Hispania.
Tangu wakati huo wamekuwa pamoja huku wakijaliwa kupata watoto wawili, Asia (2016) na Dan (2018). Maisha ya ndoa kwa Xavi yamekuwa nguzo muhimu ya utulivu na msaada katika kazi yake ya sasa.
Ndoa na familia yake vinampa msingi imara unaomwezesha kuendeleza kazi yake ya sasa ya ukocha huku akidumisha uwiano mzuri kati ya kazi na maisha binafsi baada ya kustaafu soka.
Hadi sasa tunaweza kusema ndoa yao ni ushahidi wa umuhimu wa upendo na uaminifu, pia ni uthibitisho kwamba watu maarufu na wenye mafanikio wanaweza kuwa na maisha ya binafsi yenye furaha na utulivu.
Nuria alizaliwa Novemba 9, 1981 mjini Sabadell, Hispania. Hata hivyo, hakuna taarifa nyingi kuhusu wazazi wake au ndugu zake. Hivyo haijulikani kama ni mtoto wa pekee katika familia yao au ana ndugu wengine.
Alimaliza elimu ya sekondari katika mji alikozaliwa, ambako alijulikana na wengi kama mwanafunzi bora. Tangu akiwa shule alitambua kuwa shauku yake kubwa ipo kwenye mitindo ya mavazi.
Hivyo baadaye alijiunga na Chuo Kikuu Huria huko Barcelona, Autonomous University of Barcelona ambapo alipata shahada ya Uandishi wa Habari za Mitindo (Fashion Journalism), kazi anaiyofanya sasa kwa kiasi.
Alianza kazi yake kama mwandishi wa gazeti la El Periodico de Catalunya, na mwaka 2006, alijiunga na kituo cha televisheni cha Uhispania TV3, ambapo alikuwa mtangazaji wa vipindi mbalimbali vya habari na michezo.
Kwa sasa, Nuria anajulikana zaidi kama mshawishi wa mitandao ya kijamii (social media influencer), akiwa na wafuasi zaidi ya 175, 000 katika ukurasa wake wa Instagram.
Ameongeza idadi kubwa ya wafuasi miaka ya hivi karibuni, na miongoni mwa watu maarufu wanaomfuata (follow), ni mke wa Cesc Fabregas, Daniella Semaan, pamoja na mke wa Lionel Messi, Antonella Roccuzzo.
Ingawa hupendelea maisha ya faragha, anapenda pia kushirikisha mashabiki wake matukio mbalimbali ya maisha yake hasa matukio muhimu kama sherehe.
Katika ukurasa wake, utaona ukali wake wa mitindo ya mavazi, hiyo ni kwa sababu yeye ni mtaalamu wa mitindo (fashion guru), na amekuwa akiwapa mashabiki ushauri mzuri kuhusu jinsi ya kuvaa na kupendeza.
Urefu wa Nuria ni takribani futi 5 na inchi 6, na uzito wake ni kilo 55. Ana nywele za kahawia na macho ya kahawia pia. Ana mwili wenye mvuto na afya nzuri, hasa ikizingatiwa ni mama wa watoto wawili.
Nuria amekuwa nguzo muhimu na msaada katika maisha ya Xavi, akisimama naye katika nyakati zote – nzuri na ngumu. Amekuwa akisafiri naye katika mabara na nchi mbalimbali, akimuunga mkono katika kazi yake ya soka na ukocha.
Kwa wasifu wake, ni wazi anastahili yote mazuri dunia kama Xavi ambaye alijiunga akademi ya Barcelona (La Masia) mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 11, na kucheza mechi ya kwanza kubwa dhidi ya Mallorca mnamo Agosti 1998.
Alicheza Barcelona kwa misimu 17 tena kwa mafanikio, akishinda mataji makubwa 25, yakiwamo mataji manane ya Ligi Kuu Hispania (La Liga) na manne ya Ligi ya Mabingwa Ulaya (UEFA CL).
Akiwa na timu ya taifa ya Hispania, alishinda Kombe la Dunia la FIFA la Vijana 1999, Kombe la Dunia 2010, na Kombe la Mataifa ya Ulaya (UEFA Euro) mara mbili – mwaka 2008 na 2012.
Ni mmoja wa viungo bora zaidi katika historia ya soka, ni mchezaji ambaye kazi yake inamtambulisha, kila shabiki wa soka anamfahamu. Uwezo wa kupiga pasi, kuona mbali, kutunza mpira na kujipanga uwanjani, ni vitu vilivyofanya apendwe.
Baada ya kustaafu soka, Xavi alianza kazi ya ukocha na kuwa kocha wa timu ya Al Sadd inayoshiriki Ligi Kuu ya Qatar (Qatar Stars League), ambako alifanikiwa kushinda mataji saba ndani ya kipindi cha chini ya miaka mitatu.
Mnamo Novemba 2021, aliteuliwa kuwa kocha wa timu yake ya zamani, Barcelona, na kuingoza timu hiyo kushinda Kombe la Mfalme (Copa del Rey) na Kombe la Super Cup ya Hispania. Kwa kifupi, Xavi na Nuria wamekuwa kwenye ndoa yenye upendo na mafanikio katika kazi zao.