Wito huo mkali umetolowwa leo na kundi la wazee likijumuisha viongozi wa zamani wa Umoja wa Mataifa kutokana na kuongezeka kwa mateso ya kibinadamu nchini Sudan, wakitaka hatua za haraka za kimataifa kuwalinda raia na kuharakisha mazungumzo ya amani.
Mtoto ameketi karibu na jiko la kupikia huko Tawila baada ya familia yake kutoroka El Fasher.
Janga la kibinadamu limeighubika Sudan
Wazee hao wamelaani shambulio la hivi karibuni dhidi ya jiji la El-Fasher lililofanywa na Jeshi la Wanamgambo wa kikosi cha msaada wa haraka RSF, wakisema kuwa kuna “uthibitisho mwingi wa uhalifu mkubwa, ikiwemo taarifa za ubakaji wa makundi zilizoripotiwa na Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa OHCHR”.
Wakati tangazo la baa la njaa tayari limeshatolewa na watu milioni 21 kukabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, kundi hilo limesisitiza kuwa wahusika wote katika mgogoro na washirika wao wa nje lazima wabadilike mara moja.
Wamezitaka nchi za nje zinazoendeleza mgogoro huo kusitisha uvunjaji wa vikwazo vya silaha vya Umoja wa Mataifa na kutekeleza wajibu wao wa kimataifa.
Wazee hao pia wamezitaka pande kuu zinazohusika katika vita kukubali mapendekezo ya “Quad” ambazo ni nchi nne Marekani, Umoja wa Falme za Kiarabu, Misri na Saudi Arabia ya kutangaza usitishaji wa uhasama kwa minajili ya kibinadamu kwa miezi mitatu, na kushiriki mazungumzo ya kiufundi na Umoja wa Mataifa kuhusu kupunguza mivutano na ulinzi wa raia.
Wamerudia tena wito wa kuungwa mkono kwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu kuchunguza uhalifu unaofanywa na pande zote, wakikumbusha kuwa miaka 17 baada ya kupitishwa kwa Azimio la Baraza la Usalama namba 1820, ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro bado unasambaa na bila kuadhibiwa.”
Kambi ya Shari huko Bunia, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, inatoa hifadhi kwa familia ambazo zimekimbia migogoro.
DRC mateso kwa raia yamefurutu ada
Wazee hao wameeleza hofu kubwa kuhusu athari mbaya za mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC, ambako watu karibu milioni 6 wamekimbia makazi yao na robo ya wananchi wanakabiliwa na uhaba wa chakula. Wameangazia kuongezeka kwa ukatili wa kingono unaohusiana na migogoro, wakisema kuwa kila baada ya dakika nne mwanamke anabakwa, na kila nusu saa, mtoto.
Taarifa hiyo imetoa wito kwa Rwanda kutekeleza kikamilifu Azimio la Baraza la Usalama la 2773, linalotaka kusitishwa mara moja na bila masharti kwa mapigano, kuondolewa kwa Wanajeshi wa Rwanda kutoka ardhi ya DRC, na kuvunjwa kwa tawala mbadala zisizo halali zilizoanzishwa na kundi la M23. Serikali ya DRC, wamesema, pia lazima itimize jukumu lake la kulinda raia.
Wameongeza kuwa uwajibikaji ni muhimu kukomesha mzunguko wa vurugu na kutoadhibiwa ambao umeangamiza jamii kwa miongo mingi.
Wito wa mazungumzo ya amani
Wakipongeza juhudi za Marekani, Qatar na Muungano wa Afrika, Wazee wamesisitiza kuwa mazungumzo yoyote ya amani lazima yatangulize haki za binadamu, haki za kisheria, na mamlaka ya kitaifa na si maslahi ya kibiashara.
Wameonya kuwa dunia imepuuza athari za kibinadamu za migogoro hii kwa muda mrefu sana, na wamesema kuwa hatua zitakazochukuliwa sasa na jumuiya ya kimataifa “zitajaribu ubinadamu wetu wa pamoja.”
Juan Manuel Santos, Rais wa zamani wa Colombia na Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel akihutubia Baraza la Usalama Mkutano wa baraza kuhusu vitisho kwa amani na usalama wa kimataifa athari za mabadiliko ya tabianchi. (Maktaba)
Wazee hao ni kina nani?
Wazee hao ni kundi la viongozi huru wa kimataifa wakiwemo wafanyakazi wa zamani wa Umoja wa Mataifa lilioundwa na Nelson Mandela kwa lengo la kuendeleza amani, haki na maslahi ya binadamu duniani. Miongoni mwa walioidhinisha taarifa hii ni:
- Juan Manuel Santos – Rais wa zamani wa Colombia na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel (Mwenyekiti)
- Graça Machel – Mwanzilishi wa Graça Machel Trust (Naibu Mwenyekiti)
- Gro Harlem Brundtland – Waziri Mkuu wa zamani wa Norway
- Helen Clark – Waziri Mkuu wa zamani wa New Zealand
- Elbegdorj Tsakhia – Rais na Waziri Mkuu wa zamani wa Mongolia
- Zeid Ra’ad Al Hussein – Kamishna Mkuu wa zamani wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa
- Hina Jilani – Mwanasheria na mtetezi wa haki
- Ellen Johnson Sirleaf – Rais wa zamani wa Liberia na mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel
- Denis Mukwege – Daktari na mtetezi wa haki za binadamu, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel
- Mary Robinson – Rais wa zamani wa Ireland
- Ernesto Zedillo – Rais wa zamani wa Mexico