El Fasher
Katika ziara hiyo ya siku tatu kuanzia tarehe 14 hadi 16 mwezi huu wa Novemba, Fletcher amekutana na wanawake waliokimbia El Fasher na kusimulia jinsi walivyokuwa wamezingirwa kabla ya kutoroka kwa miguu kupitia njia zilizojaa mashambulizi ya mabomu, uporaji, na ukatili wa kingono uliokithiri.
“Walituzingira kutoka pande zote,” anasema Sumaya, aliyekimbia El Fasher tarehe 25 Oktoba. “Walilenga vyanzo vya maji, masoko na mashine za kusaga. Hakuna chakula kilichoingia au kutoka. Ndege zisizo na rubani zilikuwa juu ya vichwa vyetu; kila aina ya silaha ilikuwa angani na ardhini.”
Halima, mwingine aliyotoroka, alieleza mashambulizi ya kila mara na vifo vya watoto katika mtaa wake. “Ukienda sokoni, mtoto wako hatarudi,” aanasema huku akiomba blanketi, mikeka, lishe na chakula.
Mwanamke aliyekimbia El Fasher huko Darfur akibeba msaada katika kambi ya watu waliokimbia makazi yao huko Tawila.
Tawila
Katika kambi ya wakimbizi wa ndani ya Daba Naira, eneo la Tawila, Fletcher ametembelea kituo cha kutibu utapiamlo kinachoendeshwa na shirika la Save the Children kwa msaada wa Mfuko wa Kibinadamu wa Sudan. Aliwasifu wahudumu walioko mstari wa mbele na kuwaita “mashujaa wa misaada ya kibinadamu.” Anasema, “Nimevutiwa sana na kazi yao.”
Hali ilikuwa mbaya zaidi Korma, ambako maelfu wanahifadhiwa katika kituo cha Silik. “Hiki ndicho kiini cha ukatili usio wa kibinadamu katika mgogoro huu,” Fletcher amesema. “Watu wamepambana sana ili kufika hapa… na wanapofika hawana chochote. Hii ni hali ya hatari sana, na dunia lazima itoe msaada.”
Miongoni mwa waliokimbia ni Haseena, mwalimu wa lugha ya Kiingereza aliyempoteza mwanawe wa miaka 23 mwezi Septemba na kutembea kwa siku kadhaa akitoroka vita. “Vita ni ovu, ni hatari sana,” alnasema. Fletcher alimpongeza kwa ujasiri wake na kuahidi kupeleka sauti ya jamii hiyo kwa ulimwengu.
Mratibu wa Misaada ya Dharura wa Umoja wa Mataifa, Tom Fletcher, (katikati kulia) akisafiri hadi Tawila huko Darfur.
Akutana na RSF
Fletcher pia alikutana na wawakilishi wa kundi la wapiganaji la Rapid Support Forces (RSF), akisisitiza madai ya Umoja wa Mataifa ya uwajibikaji kamili kwa ukatili uliofanyika El Fasher, ulinzi wa raia, na upatikanaji salama wa misaada ya kibinadamu kuingia na kutoka kwenye mji huo.
Tawila na Korma sasa ni maeneo makuu ya kupokea watu wanaokimbia kuzorota kwa usalama El Fasher, huku mashirika ya kibinadamu yakionya kwamba chakula, maji na dawa ni pungufu kwa kiwango cha kutisha.