Bi. Msuya ambaye amezungumza kwa niaba ya Mkuu wa OCHA, Tom Fletcher, amesema kadiri ukatili unavyoongezeka, ndivyo uhaba wa chakula unavyokuwa mbaya zaidi.

Mashambulizi dhidi ya raia, miundombinu na mashamba yamekatiza minyororo ya chakula, kupandisha bei na kuharibu maisha. Yemen, Syria na maeneo mengine yanakabiliwa na hali kama hizi, huku vizuizi vya misaada vikichochea njaa na utapiamlo.

Bi. Msuya amekumbusha kuwa sheria za kimataifa za kibinadamu zinalinda raia na zinakataza kutumia njaa kama silaha ya vita, huku Azimio 2417 likisisitiza wajibu wa pande zote zilizopo kwenye migogoro kuruhusu misaada kupita bila vikwazo.

Mkate unasambazwa katika duka la mikate huko Deir Al Balah, Gaza.

© UNOCHA/Charlotte Cans

Mkate unasambazwa katika duka la mikate huko Deir Al Balah, Gaza.

Ameonya kuwa ukosefu wa upatikanaji wa misaada unazidisha mateso, na amesisitiza kuwa katika Ukanda wa Gaza licha ya mwezi mmoja wa kusitisha mapigano vizuizi katika mipaka na ucheleweshaji wa misafara yenye misaada ya kibinadamu bado vinazuia huduma muhimu. Sudan pia inakabiliwa na mgogoro mbaya zaidi wa njaa duniani, huku mamilioni wakikosa kufikiwa na misaada.

Pamoja na mambo mengine Bi. Msuya ameitaka jamii ya kimataifa kuchukua hatua katika maeneo manne:

  1. Kutumia ushawishi kushughulikia njaa katika migogoro.
  2. Kuimarisha ulinzi wa raia na kuheshimu sheria za kimataifa.
  3. Kuwezesha upatikanaji wa misaada kwa kuondoa vikwazo vya ukiritimba.
  4. Kuimarisha uwajibikaji na uchunguzi wa ukiukaji.

Amesisitiza bila utashi wa kisiasa, juhudi za kibinadamu haziwezi kuzuia njaa inayosababishwa na vita.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *