Willemstad, Curaçao. Taifa dogo lenye watu 155,900 linalojulikana kwa jina la Curacao limefanikiwa kufuzu fainali za Kombe la Dunia mwaka 2026, ikiwa ni mara yao ya kwanza katika historia.

Taifa hilo dogo lililopo bara la Amerika ya Kusini limeweka rekodi ya kuwa taifa lenye watu wachache zaidi kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika kwa ushirikiano wa mataifa matatu, Marekani, Mexico na Canada.

Timu hiyo imefuzu usiku wa kuamkia leo baada ya mchezo wake wa mwisho kucheza dhidi ya Jamaica na kuambulia suluhu iliyowapeleka moja kwa moja kwenye fainali hizo.

Hili litakuwa taifa dogo zaidi kuwahi kushiriki Kombe la Dunia mwaka ujao baada ya sare hiyo lakini jambo la kufurahisha ni kwamba kinafundishwa na kocha mwenye uzoefu mkubwa wa soka duniani Dick Advocaat ambaye hata hivyo, hakuwepo kwenye mchezo huo wa mwisho uliofanyika nchini Jamaica.

Mholanzi huyo hakuwepo uwanjani kutokana na mke wake kuugua siku moja kabla ya mchezo huo na kuondoka kwenda nchini Uholanzi kumuuguza.

Akizungumza kabla ya mechi, alisema:

“Ni uamuzi mgumu sana kuwaacha vijana hawa hapa. Ninafanya uamuzi huu kwa moyo mzito, lakini familia inatangulia kabla ya mpira wa miguu. Nikiwa Uholanzi, nitaendelea kuwa na mawasiliano ya karibu na benchi la ufundi na nina imani kubwa na kikosi hiki.”

Na, kama ilivyoripotiwa, Advocaat alitazama sare hiyo ya 0-0 akiwa nyumbani licha ya tofauti ya muda kuifanya mechi ianze saa nane usiku kwao Uholanzi.

Wanaripoti pia kwamba aliendelea kuwasiliana kwa simu na meneja wa timu, Wouter Jansen, aliyewapa maelekezo wasaidizi Dean Gorre na Cor Pot wakati wa mapumziko, hatua iliyosaidia timu kufanikisha kufuzu Kombe la Dunia.

Gazeti la The Athletic, linasema kwamba Advocaat aliwasiliana na wachezaji baada ya mechi kupitia ujumbe mfupi alioutuma:

“Hongereni. Ajabu, safi sana! Ni safari ya aina yake.”

Kocha huyo mwenye umri wa miaka 78 aliweka historia binafsi pia kwa kuwa kocha mkongwe zaidi kuwahi kufuzu Kombe la Dunia, akivunja rekodi ya Mjerumani Otto Rehhagel aliyekuwa na miaka 71 alipoiongoza Ugiriki kwenye Kombe la Dunia 2010 Afrika Kusini.

Fainali za msimu ujao hazitakuwa za kwanza kwake, kwani Mholanzi huyo msafiri amewahi pia kuiongoza Uholanzi (1994) na Korea Kusini (2006) kwenye fainali za Kombe la Dunia.

Mbali na mafanikio yake katika timu za taifa, Advocaat ameonja mafanikio ya ngazi ya klabu kwa kutwaa mataji ya ligi kuu nchini Uholanzi (PSV Eindhoven), Scotland (Rangers) na Urusi (Zenit Saint Petersburg).

Pia aliwahi kuinoa Sunderland katika Ligi Kuu ya England, akifanikiwa kuwaokoa kushuka daraja mwishoni mwa msimu wa 2014–15 kabla ya kujiuzulu mapema Oktoba msimu uliofuata.

Curacao ambayo ipo umbali wa maili 37 kutoka Venezuela ililikuwa nchi kamili mwaka 2010 ambapo kwa miaka yote ilikuwa chini ya utawala wa Uholanzi.

Miaka kumi iliyopita, taifa hilo lilikuwa linashika nafasi ya 150 kwa ubora wa soka duniani lakini kwa sasa linashika 82.

Hii inakuwa mara ya kwanza kwa mataifa yenye idadi ndogo ya watu kufuzu Kombe la Dunia, mengine yakiwa ni Cape Verde, Uzbekistan na Jordan.

Kwenye mechi 10 za kufuzu fainali hizo, imeshinda saba ikiwa haijapoteza mchezo hata mmoja.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *