Dodoma. Mwili wa aliyekuwa msanii wa Vichekesho na Mshereheshaji nchini Emanuel Mathias (MC Pilipili) umepumzishwa kwenye nyumba yake ya milele katika makaburi ya Kilimo Kwanza Ipagala jijini Dodoma leo Alhamisi Novemba 20, 2025.
Shughuli ya kuuaga mwili wa staa huyo aliyekumbwa na mauti Jumapili imefanyika leo, huku wasanii mbalimbali wakiendelea kumlilia.
Jana mwili wake uliwasilishwa nyumbani kwao ambako waombolezaji wengi waliendelea kuonyesha upendo kwa kujitokeza kumuomboleza, lakini shughuli ya kuaga na kuzikwa kwa staa huyo inafanyika leo
Chanzo cha kifo chake bado kimeacha maswali, huku Jeshi la Polisi likibainisha kwamba staa huyo alishambuliwa kwani mwili wake umekutwa na majeraha katika sehemu mbalimbalimbali na wanaendelea na uchunguzi.
Kilichowasikitisha wengi ni kwamba taarifa hizo zinakuja wakati ambao wengi walikuwa wakimwona MC Pilipili alikuwa mtu aliyependa kufurahi wakati wote na wala kuwa na matukio ya kugombana na watu.
Pilipili anazikwa huku akiwaachia maswali si tu familia yake, bali hata mastaa wenzake ambao wengine wamefunguka namna walivyomfahamu na kufanya naye kazi wakieleza kwamba alikuwa ni mtu ambaye hakutaka kugombana na wengine.
Msemaji wa familia, Paschal Maingu, alieleza kuwa mwili wa marehemu ulikutwa na majeraha makubwa.
Paschal anasema kuwa, mdogo wa mwisho wa marehemu alimueleza kwamba, Pilipili alipitia mateso mazito kabla hajafariki.
Hali hii iliibua shaka kubwa ndani ya familia na jamii, huku uchunguzi wa polisi ukiendelea kutafuta chanzo halisi cha kifo hicho.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma, Dk Ernest Ibenzi alisema MC Pilipili alipokewa hospitalini hapo akiwa tayari amepoteza maisha na mwili ulipelekwa hapo na wasamaria wema kati ya saa 10:30 na saa 11 jioni.
Baadaye kaka yake, Christopher Matebe, alithibitisha kuwa matokeo ya uchunguzi wa awali yanaonyesha kifo cha MC Pilipili kilitokana na kupigwa na watu wasiojulikana na familia ilihitaji uchunguzi wa kina.
Akiwa kwenye mahojiano na vyombo vya habari, alishukuru uongozi wa Hospitali ya General, pamoja na Mbunge wa Dodoma Mjini, kwa kuwa karibu na familia katika kipindi hiki kigumu.