Mastaa Watano wa Simba, Yanga na Azam wameteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2024/2025.

Katika orodha iliyotolewa leo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wachezaji hao ni Dickson Job, Pacome Zouzoua, Maxi Nzengeli wa Yanga, Jean Ahoua wa Simba na Feisal Salum wa Azam FC.

Mshindi wa Tuzo hiyo atatangazwa Desemba 5, 2025 katika Hafla ya Tuzo za TFF 2024/2025 itakayofanyika hapa Dar es Salaam.

Kama ilivyo kwa nyota hao wa kiume, wachezaji watano pia wameteuliwa kuwania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania Bara msimu uliopita.

Wachezaji hao ni Donisia Minja na Stumai Abdallah (JKT Queens), Jeannine Mukandayisenga (Yanga Princess), Jentrix Shikangwa (Simba Queens) na Esther Maseke (Bunda Queens).

Tuzo ya Refa Bora wa Ligi Kuu 2024/2025 inawaniwa na Ahmed Arajiga, Saad Mrope na Abdallah Mwinyimkuu.

Upande wa Kocha Bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu uliopita, wanaowania ni Fadlu Davids aliyekuwa Simba, Rachid Taoussi aliyekuwa Azam FC na Ahmad Ally wa JKT Tanzania.

Katika Kombe la Shirikisho la CRDB, Tuzo ya Mchezaji Bora inawaniwa na Clement Mzize na Stephane Aziz Ki wa Yanga na Emmanuel Keyekeh wa Singida Black Stars.

Wachezaji Mbwana Samatta, Novatus Dismas na Saimon Msuva, wanawania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kiume anayecheza nje ya Tanzania.

Wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora wa Kike anayecheza nje ya nchi ni Opa Clement, Diana Lucas na Enekia Kasonga.

“Tuzo za Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), msimu wa mwaka 2024/2025 zimepangwa kufanyika Desemba 5, 2025 ukumbi wa The Super Dome, Dar es Salaam.

“Tuzo zitakazotolewa zimegawanyika katika makundi makuu matano, ambayo ni Tuzo za Ligi Kuu ya NBC, Tuzo za Kombe la Shirikisho la CRDB, Tuzo za Ligi Kuu ya Wanawake, Tuzo za Ligi Nyingine na

Tuzo za Utawala.

“Msimu wa 2024/25 kutakuwa na tuzo moja mpya ambayo ni Mchezaji Bora wa Tanzania Anayecheza Nie upande wa wanawake. Tuzo ya Mchezaji Bora wa Tanzania Anayecheza Nje ilitambulishwa rasmi katika sherehe za Tuzo za TFF msimu wa mwaka 2023/24, lakini ilitolewa upande wa wanaume tu,” imefafanua taarifa ya TFF.

Zaidi ya tuzo 40 zitashindaniwa katika Hafla ya Tuzo za TFF mwaka huu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *