
Dar es Salaam. Kwa miaka mingi, wanafunzi wa elimu ya juu wamekuwa wakichelewa kumaliza masomo kutokana na ugumu wa kuchapisha tafiti kwenye majarida ya kitaaluma.
Kutokana na changamoto hiyo, Chuo cha Uhasibu (IAA) imeamua kuanzisha mkutano wa kitaaluma wa wanafunzi (Academic Conference) unaowapa jukwaa mbadala la kuwasilisha tafiti na kupata mrejesho wa kitaalamu papo hapo.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 21, 2025 Mkuu wa chuo cha IAA, Profesa Eliamani Sedoyeka, wanafunzi wengi huingia kwenye hofu mara tu wanapokamilisha utafiti wao kwa sababu wanajua kwamba hatua inayofuata ni uchapishaji ndiyo ngumu zaidi.
“Mwanafunzi akishamaliza utafiti, analazimika kuchapisha. Lakini mchakato wa kutuma journal, kusubiri mrejesho, kufanya marekebisho na kupata idhini ya uchapishaji umekuwa mrefu na mgumu sana. Hii imekuwa ikichelewesha wanafunzi wengi.”amesema Profesa Sedoyeka.
Amesema katika mkutano huo, wanafunzi hupata nafasi ya kuwasilisha kazi zao mbele ya jopo la wahadhiri na wataalam, ambao huuliza maswali ya kitaaluma, kutoa changamoto na mapendekezo ya kuboresha tafiti zao.
“Hapa wanafunzi hawatetei tu mbele ya msimamizi wao, wanajenga ujasiri wa kitaaluma kwa kutetea mbele ya hadhira, wanakosolewa, wanaboresha, hiki ndicho kinachojenga watafiti wenye weledi.”
Amesema baada ya maboresho, tafiti hizo huchapishwa kwenye conference proceedings za chuo, hivyo kuwasaidia wanafunzi kukidhi sharti muhimu la kuhitimu bila kupitia michakato mirefu ya nje.
Kwa upande wake, Dk Kelvin Juna, Mkuu wa Kampasi ya IAA Dar es Salaam, anasema tafiti zinazowasilishwa hutokana moja kwa moja na changamoto halisi ndani ya jamii.
“Wanafunzi wanachukua mada kutoka kwenye maisha ya watu uchumi wa kaya, biashara ndogo mfano mama lishe, changamoto za kijamii. Hizi tafiti zina uwezo mkubwa wa kusaidia watunga sera na kuongeza uelewa wa matatizo ya wananchi.”
Amesema tafiti kama hizi, zinaweza kuwa nyenzo muhimu katika kutengeneza sera zinazogusa maisha ya wanawake wengi nchini.
Mbali na hilo, Dk Juna amesema IAA imeimarisha mfumo wa blended learning kutokana na uwekezaji wa Mradi wa Higher Education for Economic Transformation (HEET), unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, umeendelea kuleta mageuzi makubwa katika elimu ya juu nchini kwa kuboresha miundombinu, kuongeza matumizi ya TEHAMA.
“Tumepata smart classrooms, vifaa vya kisasa vya kufundishia na kufanyia utafiti. Teknolojia hii imetupa uwezo wa kufundisha wanafunzi ambao pia ni watumishi bila kuathiri ajira zao.”